"Umenirahisishia malezi" Akothee amsherehekea bintiye Fancy Makadia kwa ujumbe maalum

Muhtasari

•Akothee amemtaja bintiye kama msichana mtulivu, mwenye nidhamu, mwenye maono na mwenye kuelewa.

•Mwanamuziki huyo hata hivyo amesema anajuta sana kumtambulisha bintiye kwa 'mafisi' wa mitandaoni.

Akothee na bintiye Fancy Makadia
Akothee na bintiye Fancy Makadia
Image: HISANI

Hivi leo (Machi 21), mtoto wa tatu wa Akothee, Prudence Brina almaarufu Fancy Makadia anaadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Akothee amechukua fursa hiyo kumsherehekea bintiye huku akimtaja kama msichana mtulivu, mwenye nidhamu, mwenye maono na mwenye kuelewa.

Mama huyo wa watoto watano amesema kuwa sifa za bintiye za kupendeza zimefanya malezi yake  kuwa rahisi.

"Sijakuwa nawe miaka mitatu lakini umeendelea kuhifadhi kiwango kikubwa cha nidhamu. Siichukulii kwa urahisi. Umefanya uzazi kuwa rahisi sana kwangu. Ulielewa jukumu la kuwa mtoto nami kuwa mama. Nakupenda hadi kifo Fancy Makadia," Akothee amesema.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 42 hata hivyo amesema anajuta sana kumtambulisha bintiye kwa 'mafisi' wa mitandaoni.

Akothee amemshauri binti huyo wake ambaye alihitimu chuo kikuu hivi majuzi kutoyasikiliza maneno ya watu huku akimtahadharisha kuwa yeye ndiye mwanamke pekee anayemtakia mafanikio maishani.

"Shukran kwa kuhitimu chuo kikuu bila drama. Unapoongeza mwaka mwingine mmoja, jua kwamba mimi Esther Akoth Kokeyo ndiye mwanamke pekee anayetaka kukuona ukiwa bora kuniliko. Kheri za siku ya kuzaliwa Fancy Makadia. Siwezi kusubiri uwasili Kenya," Akothee aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Makadia ni mtoto wa tatu wa Akothee baada ya Vesha Okello na Rue Baby.