"Uwe kichwa sio mkia" Mr Seed apiga dua maalum mwanawe anapojiunga na shule

“Nenda ukajibambe, nenda ukafurahi,nakupenda sana," Seed alimwambia mwanawe.

Muhtasari

•Gold alijawa na furaha kubwa alipokuwa akijiandaa kuripoti shuleni kwa mara ya kwanza siku ya Jumatano asubuhi.

•Mr Seed alimuombea mafanikio mtoto huyo wake anapoanza safari ndefu ya elimu na kumtakia heri shuleni.

Mr Seed, Mkewe Nimo Gachuiri na mtoto wao Gold Christen
Image: INSTAGRAM// NIMO GACHUIRI

Mtoto wa mwanamuziki wa nyimbo za injili na za mapenzi, Moses Tarus Omondi almaarufu Mr Seed, Gold Christen amejiunga na shule.

Gold ambaye ni mtoto wa pekee wa Mr Seed pamoja na mke wake Nimo Gachuiri alijawa na furaha kubwa alipokuwa akijiandaa kuripoti shuleni kwa mara ya kwanza siku ya Jumatano asubuhi.

Mr Seed alichapisha video ya mtoto huyo anayeelekea kutimiza miaka mitano akiwa amevalia sare ya shule isiyothibitishwa.

"Siku ya kwanza shuleni," aliandika chini ya video hiyo.

Katika video hiyo, Gold alimbainishia mamake kwamba anafurahi sana kujiunga na shule kwa mara ya kwanza.

Mr Seed alimuombea mafanikio mtoto huyo wake anapoanza safari ndefu ya elimu na kumtakia heri shuleni.

“Nenda ukajibambe, nenda ukafurahi,nakupenda sana," Seed alimwambia mwanawe.

"Mungu akubariki, mungu akulinde, mungu awe nawe, wewe ni mvulana uliyebarikiwa, nenda uwe kichwa na sio mkia,nakubariki wewe katika jina la Yesu,”

Mwimbaji huyo wa zamani wa EMB Records pia aliomba mwanawe  apate marafiki na awe na uhusiano mzuri na mwalimu wake.

Siku kadhaa zilizopita, Mr Seed akiwa kwenye mahojiano na Nicholus Kioko alidokeza mpango wa mwanawe kujiunga na shule.

Mwimbaji huyo alisema mwanawe anakaribia kujiunga na shule ya msingi na kueleza kuwa tayari wamefanya mipango.

"Jana ndio tulikuwa tunapima sare yake ya shule. Yaani yeye kuingia tu shule, pesa nimelipa imesimamia karo ya masomo yangu yote maishani," alisema mapema mwezi huu.

Seed alidokeza kuwa Gold Christen atajiunga na shule ya hadhi kwani nia yake ni kuwapa watoto wake maisha mazuri.

Pia alifichua kwamba alitumia hela nyingi sana ili mwanawe kujiunga na shule.