Mwanasosholaiti maarufu wa Kenya Vera Sidika Mung’asia amedokeza kuhusu kutowahi kujitosa kwenye ndoa tena.
Wakati akiwashirikisha mashabiki wake katika kipindi cha Maswali na Majibu kwenye mtandao wa Instagram siku ya Jumatano, mrembo huyo mwenye umri wa miaka 34 alibainisha kuwa alijaribu kutulia kwenye ndoa lakini haikufaulu kwake.
Mama huyo wa watoto wawili alitoa maoni hayo wakati alipokuwa akijibu shinikizo la kutulia kwenye ndoa kama sosholaiti mwenzake, Zari Hassan ambaye alifunga ndoa rasmi na mpenzi wake Shakib Cham Lutaaya mwaka jana.
“Huwezi kutulia kama Zarithebosslady. Alipata upendo na amani,” shabiki mmoja alimwandikia Vera Jumatano.
Katika majibu yake, mwanasosholaiti huyo ambaye anajulikana sana kwa makalio yake makubwa aliweka wazi kuwa alimalizana na ndoa mnamo 2023.
Pia alimpongeza Zari kwa kufanikiwa kutulia kwenye ndoa lakini akabainisha kuwa hatua hiyo haiwezekani kwake.
“Nzuri kwake. Nilijaribu. Sio ya kwangu, "alisema.
Zari na Shakib walirasimisha ndoa yao katika harusi ya faragha iliyofanyika nchini Afrika Kusini mnamo Oktoba 3, 2023. Wawili hao walikuwa wakichumbiana kwa zaidi ya mwaka mmoja kabla ya kufunga ndoa rasmi.
Vera pia alikuwa amefunga ndoa rasmi na mzazi mwenzake Brown Mauzo mnamo Oktoba 2020 kabla ya kuthibitisha kutengana mwaka jana.
Siku chache zilizopita, mwanasoshalaiti huyo aliyezingirwa na drama aliwaacha wengi katika hali ya mshangao baada ya kuandaa tafrija kubwa kwa ajili tu ya kusherehekea kuvunjika kwa ndoa yake mwezi Septemba mwaka jana.
Sidika kupitia ukurasa wake wa Instagram alipakia mfululizo wa picha na video akionyesha jinsi aliwasili katika tafrija hilo kubwa aliambatanisha na ujumbe mkuu kuhusu tafrija hilo.
Sidika ambaye alikuwa ameoleka kwa msanii Brown Mauzo kwa kipindi cha miaka 3 na kupata watoto wawili pamoja aliwataarifu mashabiki wake kwamba ameamua kuandaa bonge la tafrija kusherehekea kuvunjika kwa ndoa, akisema ndoa ni utapeli mkubwa sana kuwahi kutokea katika maisha yake.
“Tafrija ya kusherehekea talaka inakuja, ndoa ni utapeli,” aliandika Sidika kwenye insta story yake.
Mama huyo wa watoto wawili – Asia Brown na Ice Brown – alionekana akishuka kwenye gari bichi nyakati za usiku huku amezingirwa na mabaunsa na kuzindikizwa kwenye ukumbi mkuu kulikoandaliwa tafrija hiyo.