Tamasha la mwimbaji wa Kenya Willy Paul nchini Saudi Arabia mnamo Jumamosi usiku lilitatizika baada ya vita kati ya Wakenya na Waganda kuzuka.
Kulingana na mwimbaji huyo wa nyimbo za mapenzi, tiketi zote za tamasha hilo zilikuwa zimeuzwa kabla ya hali kugeuka kuwa mbaya na hivyo kusababisha shoo kutoendelea.
Mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili aliwalaumu waandaaji wa hafla hiyo kwa kuvuruga ratiba ya matukio, akidokeza kwamba ndiyo sababu ya vita kuzuka.
“Jana Usiku nchini Saudi Arabia ulikuwa Usiku Wa Huzuni Zaid maishani mwangu. Kila Kitu Kilikuwa Poa Mpaka Wakenya na Waganda Wakaanza Kupigana. Usimamizi wa Tamasha Ulifanya Kosa Kubwa. Nilikuwa Tayari Kutumbuiza Kuanzia Saa sita usiku Lakini Promota Alinipeleka Kwenye Jukwaa Saa kumi asubuhi 😔 Nikiwa na Ndugu yangu Lil Pazo Kutoka Uganda,” Willy Paul alisema katika taarifa aliyochapisha kwenye Instagram Jumapili asubuhi.
Msanii huyo mwenye sauti ya kusisimua aliambatanisha taarifa yake na video inayoangazia matukio ya fujo ya tamasha hilo lililokatizwa.
“Lil Pazo Alipopanda Jukwaani, Wakenya Walimrushia Kila Kitu Wakimfanya Aondoke Jukwaani. Hatimaye Nilipopanda Jukwaani Wakenya Walifurahi Lakini Sio Waganda, Hivyo Waganda Walinitupia Kila Kitu Walichokuwa nacho,” alisema.
Willy Paul alifichua kuwa baadhi ya mashabiki walijeruhiwa katikati ya machafuko hayo na kuwasihi watu wa Afrika Mashariki kutochukulia vita kama suluhu.
“Ilikuwa Ni Tukio Mbaya Sana. Majeraha Madogo… Vita vya Waafrika Mashariki Sio Suluhu ya Kila Kitu. Nawapenda Nyote,” alisema.
Mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za Injili ambaye hivi majuzi amekuwa kwenye ziara ya kimuziki sehemu mbalimbali duniani alitarajiwa kutumbuiza nchini Saudi Arabia usiku wa kuamkia Jumapili kwenye tamasha la Gold Party lililokuwa na lengo la kuwaunganisha mashabiki wa Afrika.