Wahu avunja kimya baada ya kukejeliwa kwa uzito wa mwili wake

Wahu alijifungua mtoto wake wa tatu mnamo Oktoba 11, 2022.

Muhtasari

•Pichani, Wahu alionekana mnene kuliko siku za hapo awali, kitu ambacho kiliwafanya baadhi ya wanamtandao kumdhihaki.

•Mwimbaji huyo pia alibainisha kwamba maneno ya chuki yaliyosemwa kuhusu mwili wake hayakufanya ahisi vibaya

Image: FACEBOOK// WAHU KAGWI

Mwanamuziki Wahu Kagwi amesikitishwa na wanamitandao waliomdhihaki kwa uzani wake wa mwili ulioongezeka baada ya kuchapisha picha yake.

Siku ya Jumatatu, mama huyo wa watoto watatu alichapisha picha yake akiwa katika mkutano wa kamati ya Talanta Initiative ambayo aliteuliwa kuwa mwanachama na waziri wa Michezo na Sanaa Ababu Namwamba.Pichani, alionekana mnene kuliko siku za hapo awali, kitu ambacho kiliwafanya baadhi ya wanamtandao kumdhihaki.

Katika taarifa yake, Wahu amethibitisha kuwa kwa kweli aliongeza kilo zaidi ya ishirini wakati wa ujauzito wake wa hivi majuzi.

"Hakika nimeongeza uzito... kilo 22.5  kuwa halisi. Kiukweli, kwa wanaonifahamu wanajua huwa naongeza uzito wakati wa ujauzito.  Nikiwa na Tumiso niliongeza 27kgs ," alisema kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Mke huyo wa mwimbaji David Mathenge almaarufu Nameless alibainisha kuwa licha ya maoni kadhaa hasi kutolewa dhidi ya mwili wake, kuna baadhi ya wanamitandao ambao walitoa maoni mazuri chini ya chapisho lake.

"Mfano mkubwa wa wema hupita ubaya. Kiasi kwamba wengi wa "wanyanyasaji" waliishia kufuta maoni yao," alibainisha.

Wahu aliendelea kuwashukuru wote ambao walijiepusha na kumkejeli na kutoa maoni mazuri kuhusu picha hiyo.

Aidha alitumia fursa hiyo kuwatia moyo watu wote ambao wamewahi kukabiliwa na unyanyasaji wa mitandaoni kwa sababu ya miili yao huku akiwataka kutohisi vibaya kwa sababu ya maoni mabaya ya wengine.

"Kumbuka, wanachosema wenye kuaibisha mwili sio wewe. Ni onyesho la ubora wako. Wewe uko tu sawa. Usichukulie uhasi moyoni,"

Mwimbaji huyo pia alibainisha kwamba maneno ya chuki yaliyosemwa kuhusu mwili wake hayakufanya ahisi vibaya

"Ninasema haya ili tutambue kuwa kuna matumaini ya mazingira mazuri zaidi ya kuishi na pia kumtia moyo mtu yeyote ambaye amekuwa mwathirika wa aina yoyote ya chuki. vinginevyo laleni fiti," alisema.

Wahu alijifungua mtoto wake wa tatu mnamo Oktoba 11, 2022.