Wema Sepetu apandwa na mori baada ya 'ex' kudai alimtoa jela na kumpa nyumba anayoishi na Whozu

Wema alibainisha kuwa huo ulimpandisha mori sana na hivyo akaamua kujibu.

Muhtasari

•PCK aliibua madai kuwa Wema Sepetu amekuwa akiumiza moyo wake kwa miaka mingi kwa kujibu wema wake kwa uovu.

•Wema alikanusha madai ya PCK akibainisha kwamba hana uwezo wa kumpa nyumba.

Image: INSTAGRAM// WEMA SEPETU

Muigizaji Wema Sepetu amemjibu kwa hasira mwanaume anayedai kuwa alimtoa jela na kumpa jumba lake moja la kifahari aishi.

PCK, kama anavyojitambulisha kwenye Instagram aliibua madai kuwa mpenzi huyo wa zamani wa mwanamuziki Diamond Platnumz amekuwa akiumiza moyo wake kwa miaka mingi kwa kujibu wema wake kwa uovu.

Mwanaume huyo ambaye anadai kuwa mpenzi wa zamani wa Wema Sepetu alisema kwamba alimtoa jela muigizaji huyo baada ya mwanamume mwingine aliyekuwa na uhusiano naye kumfanya afungwe.

"Lakini mbona bado unanifatilia? Mbona bado  unaniongelea upuuzi kwa watu wako wa karibu?" Jamaa huyo alihoji.

PCK pia alidai kuwa aliingilia kati wakati muigizaji huyo alikuwa amefilisika na kuhamia katika eneo la Mbagala.

Alidai kuwa alimfukuza mpangaji wake mmoja na kumpa Wema ili apate kwa kuishi huku akijenga upya maisha yake.

"Nilitoa mpangaji kwenye nyumna yangu huko Mbweni ambayo nilikuwa nalipwa 3000$ kwa mwezi lakini nilimtoa Mchina wa watu kwa haraka akaondoka nikakupa wewe nyumba uishi nikakununulia kila kitu cha ndani ili uanza maisha lakini shukrani yako nikunilipa kwa ubaya kila siku," alisema.

Aidha alidai kuwa nyumba aliyomuazima Wema Sepetu bila kudai kodi yoyote ni ile ile anayoishi na mpenzi wake wa sasa Whozu, kitu ambacho anasema kinamuumiza sana moyoni.

Zaidi alimuagiza muigizaji huyo kuondoka katika nyumba hiyo aliyodai ni yake na kumpa siku saba kuhamia kwingine.

"Kama ni wema wangu kwako tayari umeshaniponza. Ninachokuomba tu kiustaarabu ondoka kwenye nyumba yangu ninakupa siku saba pekee ujipange kwa kwenda lakini nahitaji nyumba yangu katika siku 7 tafadhali,"

Wema alichapisha tena ujumbe wa PCK kwenye ukurasa wake na kumjibu kwa hasira akimtaka kukoma kumuongelea.

"Ulivyokamatwa na kufanyiwa unyama na wanaume wenzako na nikakuachia suala ya kunidhulumu 32,000$ usichukulie poa," aliandika.

Muigizaji huyo pia alikanusha madai ya PCK akibainisha kwamba hata hana uwezo wa kumpa nyumba.

"Hata muda wa kukuongelesha sina. Ulifurahia spotlight ya muda mchache ukanogewa eeh, rudisha pesa yang fisi wewe," 

Wema alibainisha kuwa ujumbe wa PCK ulimpandisha mori sana na hivyo akaamua kujibu.