Zari afunguka kuolewa kutokana na shinikizo baada ya Akothee kufanya harusi

Mwanasoshalaiti huyo wa Uganda amethibitisha kufunga ndoa (Nikah) na mpenzi wake Shakib Cham Lutaaya.

Muhtasari

•Zari aliweka wazi kwamba Nikah yake iliwazwa na kupangwa vyema kabla ya kufanyika huku akiwasuta wakosoaji wa ndoa yake.

•Madai yaliibuka kuwa mwanasosholaiti huyo wa Uganda huenda alikubali shinikizo baada ya kuona harusi ya Akothee.

Zari Hassan, Shakib, Dennis Shweizer, Akothee
Image: HISANI

Mwanasosholaiti maarufu kutoka Uganda, Zari Hassan amethibitisha kufunga ndoa (Nikah) na mpenzi wake Shakib Cham Lutaaya.

Akizungumza kwenye video aliyochapisha kwenye akaunti yake ya mtandao wa Snapchat, mzazi mwenza huyo wa zamani wa staa wa Bongo Diamond Platnumz alitupilia mbali tetesi kuwa hatua hiyo ilitokana na shinikizo.

Zari aliweka wazi kwamba Nikah yake iliwazwa na kupangwa vyema kabla ya kufanyika huku akiwasuta wakosoaji wa ndoa yake.

"Mimi kuolewa kwa hakika ilichukulia vizuri na watu wengi lakini kila wakati kuna kundi la watu ambao wataelekeza masaibu yao kwangu," alilalamika.

Aliongeza, "Kila kitu kiko mahali na ndio tulifanya Nikah. Na si kwa sababu ya shinikizo, sishindani na mtu yeyote. Sasa kwa sababu tu mtu katika nchi nyingine alifunga ndoa, watu hawapaswi kuolewa tena. Je, alikuwa wa kwanza kuolewa?”

Mama huyo wa watoto watano alihoji ni kwa nini mambo ya kawaida yanapotokea katika maisha yake huwa suala miongoni mwa wanajamii.

Zari Hassan na Shakib walifunga ndoa ya Kiislamu almaarufu Nikkah wikendi iliyopita baada ya kuchumbiana kwa takribani mwaka mmoja.

Wawili hao walivishana pete usiku wa manane kuamkia Jumatatu katika hafla ya faraghani ambayo ilihudhuriwa na idadi ndogo ya watu.

Katika picha na video hafla hiyo iliyofanyika chumbani ambazo zilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii, wapenzi hao walionekana wamevalia Kiislamu kabisa huku wote wakiwa wameketi kwenye mkeka uliotandikwa sakafuni.

Shakib alionekana akiinama kwa goti moja na kumvisha Zari pete ya ndoa kwa furaha kabla ya wawili hao kupigana mabusu huku watu wachache waliohudhuria hafla hiyo wakiwasherehekea kwa makofi.

Vyanzo vya habari kutoka Uganda vilidai kwamba baada ya kuvishana pete katika tukio la faraghani, wawili hao ambao wamekuwa marafiki kwa zaidi ya miaka minne waliweka Nikkah yao bayana kwa wazazi wa Zari.

Nikah ya Zari Hassan na mpenzi huyo wake mdogo kiumri ilifanyika takriban wiki moja tu baada ya mwimbaji wa Kenya Esther Akoth almaarufu Akothee kufunga pingu za maisha na mchumba wake, Denis Shweizer (Omosh).

Madai yaliibuka kuwa mwanasosholaiti huyo wa Uganda mwenye umri wa miaka 42 huenda alikubali shinikizo baada ya kuona harusi ya Akothee. Wawili hao wana mambo mengi yanayofanana ikiwa ni pamoja na; Wote wana watoto watano, wana zaidi ya miaka 40, ni wasanii na wafanya biashara, Wamewahi kuchumbiana na wanaume wadogo ki umri, Wamewahi kuchumbiana na raia wa kigeni, wamefunga ndoa angalau mara mbili na wote wamefanya harusi mwezi Aprili.