Zari Hassan afunguka suala la kuhamia Kenya

Muhtasari

•Zari alieleza kuwa amezuru kwa ajili ya uzinduzi wa jumba  la kipekee ambalo limejengwa jijini Nairobi.

•Mwanasoshalaiti huyo alifichua kwamba anakipenda sana chakula cha hapa Kenya na kusema kuwa anakipeza.

Image: INSTAGRAM// ZARI HASSAN

Mwanasoshalaiti na mfanyibiashara mashuhuri kutoka Uganda Zari Hassan yupo nchini Kenya.

Zari alitua katika uwanja wa ndege wa JKIA Jumatano asubuhi akiwa ameandamana na walinzi wake. Alilakiwa na wanandoa Kabi na Milly Wajesus pamoja na kundi la waandishi wa habari.

Akizungumza baada ya kuwasili nchini, Zari alieleza kuwa amezuru kwa ajili ya uzinduzi wa jumba  la kipekee ambalo limejengwa jijini Nairobi.

"Mimi napenda mali. Nilitaka kujua ni nani anajenga jumba hilo. Tulianza kuwasiliana nao na tukaamua kuchukua mradi huu," Zari alisema katika mahojiano na Eve Mungai.

Wakati wa ziara yake hapa Kenya, mama huyo wa watoto watano pia ataandaa karamu ya kifahari na kufanya miradi kadhaa  ya hisani.

Zari ambaye amewahi kuishi katika nchi tatu za Afrika hata hivyo hakubainisha kipindi anachokusudia kukaa hapa nchini.

"Sijui nitakaa Kenya muda gani. Naweza kuishi milele. Kenya ni kuzuri. Nahisi vizuri hapa," Zari alisema.

Mwanasoshalaiti huyo alifichua kwamba anakipenda sana chakula cha hapa Kenya na kusema kuwa anakipeza.

"Napenda chakula cha Kenya. Napenda ugali, nyama choma na sukumawiki. Hiyo ni lazima na sijazikula kwa muda mrefu," Alisema.

Zari hakutupilia mbali uwezekano wa kuwahi kuishi Kenya huku akibainisha kuwa hapa ni kama nyumbani kwake pia.

"Sijui lakini kila kitu chawezekana. Mimi ni Mwafrika Mashariki, Kenya ni sehemu ya Afrika Mashariki. Chochote chaweza kutokea," Alisema.

Miaka ya hapo awali Zari ambaye kwa sasa anaishi Afrika Kusini amewahi kuishi Uganda (nchi ya kuzaliwa) na Tanzania ambako alikuwa ameolewa.