BUSIA: Polisi Wasaka Mfungwa Aliyetoroka Gerezani

picha: indybay.org | 

Maafisa wa usalama katika kaunti ya Busia wameanzisha msako dhidi ya mfungwa mmoja aliyetoroka kutoka kwa gereza la Korinda.

Mfungwa huyo anadaiwa kutoroka kutoka gereza hilo katika hali ya kutatanisha sana.

Akithibitisha kutoweka kwa mfungwa huyo, kamishna wa kaunti ya Busia, Bw. Mongo Chimwaga, amesema kuwa mshukiwa anadaiwa kutoroka walipokuwa wakifanya kazi katika shamba la gereza hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Busia, Mongo alidokeza kuwa msako huo unahusisha vitengo vyote vya usalama katika kaunti hiyo ili kunasa mshukiwa huyo ambaye alikuwa anahudumu kifungo cha miaka miwili.

Vile vile, amewarai wananchi kusaidia polisi katika juhudi za kusaka mfungwa huyo kwa kupeana habari muhimu kumhusu.