Carabao: Mashetani wekundu kumenyana na Chelsea, Liverpool kukabana na Arsenal

carabao cup
carabao cup
Manchester United walihitaji penalty ili kuibandua timu ya League one Rochdale na kufuzu kwa raundi ifuatayo ya kombe la Carabao.

Pande hizo mbili zilitoka sare ya 1-1 kabla ya United kushinda mabao 5-3 kupitia kwa mikwaju ya penalty. United watakabana na Chelsea katika raundi ya nne Oktoba tarehe 28, baada ya the Blues kuwanyuka Grimsby.

Kwingineko Liverpool waliwanyuka MK Dons mabao 2-0 na sasa watachuana na Arsenal ugani Anfield. Manchester City nao watacheza dhidi ya Southampton.

Real Madrid waliendeleza msururu wa kutoshindwa katika La Liga kwa kuwanyuka Osasuna 2-0 na kuregea kileleni mwa jedwali. Meneja Zinedine Zidane aliwapumzisha baadhi ya wacheza wa kikosi cha kwanza akiwemo Gareth Bale, kabla ya derby ya Madrid na Atletico siku ya Jumamosi.

Real, ambao wameshinda mechi za ligi nne na kutoka sare moja, wako kileleni wakiwa na alama 14, mbele ya Atletico ambao wako katika nafasi ya pili.

Aliyekuwa nahodha wa Barcelona Carles Puyol amekataa fursa ya kuwa mkurugenzi wa spoti wa klabu hiyo. Miamba hao wa Uhispania walizungumza na Puyol mwenye umri wa miaka 41, aliyestaafu kama mchezaji mwaka wa 2014, kuhusu kujiunga nao tena katika wadhfa wa usimamizi.

Puyol aliondoka mwaka wa 2015 baada ya kuhudumu kidogo kama msaidizi wa mkurugenzi wa spoti wakati huo.

Tukirudi humu nchini, afisa mkuu wa KPL Jack Oguda anasema KPL inaweza kujimudu inapoendelea kutafuta wafadhili. KPL ilianza msimu bila ya wafadhili baada ya sportpesa kusitisha mkataba wao, kufuatia kufutwa kwa leseni yao.

Bado wanasubiri kampuni hio ya kamari kupata leseni mpya kabla ya kujadili mkataba mpya. Hata hivyo Oguda anasema vilabu vina njia zake za kupata mapato, kwani fedha za wafadhili huwa hazitoshi.