Carlo Ancellotti ateuliwa kocha wa Everton

Ancelotti anatua Everton siku chache baada ya kutimuliwa katika klabu ya Napoli ya nchini kwao Italia.

Anachukua nafasi iliyoachwa wazi katika uga wa Goodison Park na kocha Marco Silva ambaye alitimuliwa Disemba 6.

Ancellotti ni moja ya makocha wenye mafanikio makubwa barani Ulaya, amenyakua Kombe la Klabu Bingwa Ulaya (Champions League) mara tatu.

Anarejea England miaka nane na nusu toka alipotimuliwa na klabu ya Chelsea.

"Kuna maono ya wazi kabisa kutoka kwa mmiliki kuwa anataka kuleta mafanikio klabuni," amesema Ancelotti.

Everton wamemtangaza Ancelotti saa chache kabla ya mchezo wao dhidi ya Arsenal ambao Ijumaa walimteua Mikel Arteta kuwa kocha wao mpya.

Mechi yake ya kwanza kuiongoza timu hiyo itakuwa dhidi ya Burnley Disemba 26.

"Hii ni klabu nzuri na yenye utajiri wa historia na mashabiki wenye mapenzi ya juu," ameeleza kocha huyo wa zamani wa AC Milan, Real Madrid, Bayern Munich na Paris St-Germain.

"Nina furaha isiyo na kifani kwa kupata nafasi ya kufanya kazi hapa na kuffanya ndoto zetu zitimie."

Katika miaka yake 24 ya ukocha, Ancelotti mwenye miaka 60 ameshinda mataji 15, na ni moja kati ya makocha watatu tu ambao wameshinda Champions League mara tau sawa na kocha nguli wa zamani wa klabu ya Liverpool Bob Paisley na kocha wa sasa wa Real Madrid Zinedine Zidane.