Champions league: Barcelona, Dortmund na Inter Milan kumenayana

champions league
champions league
Liverpool watakabana na Napoli, Salzburg na Genk katika awamu ya makundi ya Champions League msimu huu. Mabingwa wa ligi ya Premier Manchester City watapambana na Shakhtar Donetsk, Dinamo Zagreb na Atlanta.

Tottenham wako katika kundi B na Bayern Munich, Olympiakos na Red Star Belgrade. Chelsea nao wako katika kundi moja na Ajax, Valencia na Lille.

Paris St-Germain na Real Madrid wamewekwa katika kundi A huku Barcelona, Borussia Dortmund na Inter Milan watakutana katika kundi F. Michuano ya makundi inaanza jumanne tarehe 17 Septemba.

Hayo yakijiri, mshambuliaji wa LA Galaxy Zlatan Ibrahimovic amesema yupo tayari kurejea klabu yake ya zamani ya Manchester United mwezi Novemba.

Mshambuliaji huyo mkongwe mwenye miaka 37 amepachika magoli 46 katika michezo 49 toka alipohamia kwenye ligi ya Marekani (MLS) mwezi Machi 2018.

"Ninaweza kucheza kwa urahisi kabisa katika Ligi ya Primia. Hivyo, kama United watanihitaji, nipo tayari," amesema.

Ibrahimovic aliifungia Man United magoli 28 msimu wa 2016-17 kabla ya kuandamwa na majeraha ya goti.

Mkataba wake wa miaka miwili na klabu ya United ulivunjwa kwa pande zote mbili kuridhia na kumruhusu kwenda Marekani.

Hata hivyo, endapo atafanikiwa kurejea United, atalazimika kusubiri mpaka mwezi Januari ambapo dirisha la usajili kwa ligi ya Uingereza litafunguliwa.

"Nimefanya kazi yangu Ulaya. Niliifurahia, nina mataji 33 ambayo nimeyashinda kule, na ninaamini nitashinda kitu hapa.

"Baada ya hapo tutaona nini kitafuata na safari itaishia wapi."

Ibrahimovic amesema kuwa anaendelea kuangalia mechi za Manchester United na kusisitiza kuwa walikosa bahati walipofungwa na Crystal Palace Jumamosi.

Marcus Rashford alikosa penati wakifungwa na Palace, kama ilivyotokea kwa Paul Pogba wakati wa sare na Wolves siku tano kabla.

"Nimeangalia mchezo wa mwisho na naamini hawakuwa na bahati tu," amesema.

"Kama wakipata penati unakuwa mchezo wa tofauti kabisa, lakini mchezo nchini England hukamilika pale tu kipyenga cha mwisho kinapolia.

"Kitu chochote kinaweza kutokea, hususani katika dakika za mwisho wakati joto hupanda kweli kweli."

-BBC