Champions league: Liverpool wapoteza, Dortmund yaadhibu PSG

atletico
atletico
Liverpool jana ilipoteza 1-0 katika mkondo wa kwanza wa raundi ya 16 ya michuano ya ligi ya mabingwa mikononi mwa Atletico Madrid ugani Wanda Metropolitan.

The Reds ambao wamekuwa katika fomu nzuri walipewa dozi wakati Atletico walipowatoa kijasho kwa kuwazuia kufunga. Mohamed Salah, na Jordan Henderson walikosa nafasi hizo.

Kwingineko Erling Haaland aliendeleza ufungaji mabao msimu huu kwa kuongeza mawili na kuwapa Borussia Dortmund ushindi wa 2-1 dhidi ya Paris St-Germain.

Mino Raiola anapanga kufanya mazungumzo na meneja wa Manchester United Ole Gunnar Solskjaer, akisisitiza hakuna mkwaruzano kati yao, kufuatia matamashi aliyoyatoa kuhusu Paul Pogba.

Raiola, ambaye ni ajenti wa kiungo huyo aliandika kwenye mitandao ya kijamii kuwa Pogba si mali yake wala ya Solskjaer, baada ya meneja huyo wa United awali kusema kua Paul ni mchezaji wake na sio wa Mino.

Solskjaer aliulizwa kutoa maoni yake kuhusu matamshi ya Mino na akasema huenda hatazungumza na Pogba au Raiola kuhusu suala hilo. Pogba anaendelea kuhusishwa na uhamisho kutoka Old Trafford.

Son Heung-Min wa Tottenham atakosa muda wa msimu uliosalia baada ya kuvunjika mkono dhidi ya Aston Villa jumapili.

Son atalazimika kufanyiwa upasuaji kwa jeraha hilo alilolipata baada ya kugongana na Ezri Konsa wa Villa. Taarifa kutoka Tottenham zinasema kuwa atakosa wiki kadha lakini Jose Mourinho anasema huenda isiwe hivyo. Son amekuwa mchezaji wao anayetegemewa zaidi tangu Harry Kane kukaa nje, akiwa amefunga mabao sita katika mechi tano alizocheza mwisho.

Kiungo Mfaransa Matteo Guendouzi mwenye umri wa miaka 20, anakabiliwa na mapambano ya kusalia katika klabu ya Arsenal, baaada ya kuachwa kwenye kikosi cha klabu hiyo kwenye mchezo wa Jumapili dhidi ya Newcastle.

Guendouzi aliachwa baada ya kugombana na kocha wa Arsenal Mikel Arteta na makocha wasaidizi wakati wa mapumziko mafupi ya katikati ya msimu jijini Dubai.

Zaidi ya vilabu elfu 1 vimeratibiwa kushiriki uchaguzi wa kaunti na wa kitaifa baada ya bodi ya FKF kuchapisha orodha ya mwisho ya watakaoshiriki chaguzi hizo. Hii ni baada ya kutamatika kwa muda wa kusuluhisha mizozo kuhusu orodha ya awali iliyochapishwa tarehe 6 mwezi huu. Orodha hio inajumuisha vilabu elfu 1,014 ambavyo vimeshiriki ligi za FKF katika angala misimu mitatu kati ya minne iliyopita. Soka ya kinadada itawasilishwa na vilabu vitano.