Champions league: Suarez aokoa Barcelona, Liverpool na Chelsea wapata ushindi

suarez
suarez
Luis Suarez alifunga mabao mawili Barcelona walipotoka nyuma na kuwanyuka Inter Milan 2-1 katika mechi ya ligi ya mabingwa.

Lautaro Martinez aliwapa vijana wa Antonio Conte bao la uongozi na kukaribia kufunga la pili pia. Suarez akasawazisha na mpira kutoka kwa pasi ya Arturo Vidal.  Lionel Messi katika mechi yake ya kuregea kutoka kwa jeraha alimpata Suarez ambaye mkiki wake ulimpita Diego Godin na kuingia wavuni.

Haya yallikuwa mabao mawili ya kwanza ya Suarez katika ligi ya mabingwa katika kipindi cha zaidi ya miaka mitatu.

Liverpool jana walijikakamua dhidi ya Salzburg na kushinda mabao 4-3 katika mechi ya awamu ya makundi ya ligi ya mabingwa. The Reds waliongoza 3-1 kufikia muda wa mapumziko lakini wageni wakafunga mabao zaidi na kusawazisha kabla ya Mohammed Salah kufunga bao la kuwapa ushindi.

Kwingineko Chelsea waliwanyuka Lille mabao 2-1 huku Barcelona wakifunga Inter Milan 2-1.

Kiungo wa kati wa Manchester United Paul Pogba atakosa mechi ya leo ya ligi ya Uropa dhidi ya AZ Alkmaar kutokana na jeraha la mguu. Pogba alicheza dhidi ya Rochdale katika kombe la Carabao na ya ligi ya Primia dhidi ya Arsenal, lakini anakabiliwa na matatizo ya mguu.

Wing'a Anthony Martial na walinzi Luke Shaw, Phil Jones na Aaron Wan-Bissaka pia wataikosa mechi hiyo lakini kinda Brandon Williams amejumusihwa. Diogo Dalot na Angel Gomes pia watacheza lakini Pogba ni pengo kubwa kwa kikosi cha Ole Gunnar Solskjaer.

Tukirejea humu nchini, Hellen Obiri anasema yuko asilimia 90 tayari kwa fainali ya jumamosi ya mbio za mita elfu 5 kwa kinadada katika mashindano yanayoendelea ya ubingwa wa dunia. Obiri alifuzu jana kwa urahisi na anasema yuko tayari kutetea taji lake baada ya kutoshinda katika mbio za mita elfu 10.

Wachezaji raga waliosusia kucheza msimu uliopita kwa kulalamikia malipo, wameregelea mazoezi wakati kocha wa Kenya Sevens Paul Feeney akijitayarisha kuchagua kikosi kitakachoshiriki Safari Sevens wiki ijayo.

Collins Injera, Billy Odhiambo na Willy Ambaka ni miongoni mwa wachezaji walioregelea mazoezi. Wengine ni Leonard Mugaisi, Augustine Lugonzo, Bush Mwale na Jeff Oluoch. Wachezaji wengine kama vile Eden Agero na Oscar Ouma bado hawajaregea.