Chanjo itakayomaliza maambukizi mapya ya HIV yazinduliwa

Kituo cha udhibiti wa magonjwa na maambukizi kimeannza kuifanyia kazi chanjo ya virusi vya Ukimwi ambayo itasaidia kumaliza maambukizi mapya ya HIV nchini Kenya, kulingana na BBC.

Chanjo hiyo kwa jina HPTN-081 ni kinga inayohusisha protini ya damu inayoweza kupigana dhidi ya virusi vya HIV.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya 40 ya kituo hicho kwa ushirikiano na Kenyaa mjini Kisumu siku ya Ijumaa, Mkurugenzi mkuu wa kituo hicho nchini Kenya Marc Bultery alisema kwamba utafiti utahakikisha kuwa chanjo hiyo inaweza kusambazwa hadi maeneo mengine.

Tayari tumemailiza vipimo vyetu vya awamu tatu za chanjo hiyo na tunaelekea katika kupiga hatua kubwa zaidi ambazo zinaweza kwa kamili kuzuia virusi vya HIV, alisema Bultery.

''Tunaangazia wanawake kwasababu ni miongoni mwa makundi yalio na hatari kubwa ya kuambukizwa'', alinukuliwa na Daily Nation akisema.

Daktari Bultery pia alisema kwamba kituo hicho kitasaidia katika mpango wa afya kwa wote nchini Kenya UHC.

''Ni lengo letu kuhakikisha kuwa makundi yote yanaweza kupata matibabu ya bure ikiwemo makundi yaliobaguliwa kama vile wapenzi wa jinsia moja'', alisema bwana Bultery.

Naibu mjumbe maalum wa Marekani nchini Kenya Eric Kneedler alisema kwamba serikali ya Marekani imejizatiti kusaidia mpango wa afya kwa wote ikiwa miongoni mwa ajenda nne za serikali.

''Lengo ni kuona kwamba serikali ya Kenya inakuwa kutoka katika taifa linalotarajia kufaidika hadi taifa lililofaidika'', alisema bwana Kneedler.

Sherehe hizo za maadhimisho zilifanyika kukumbuka mafanikio yakituo hicho nchini Kenya kwa kipindi cha miaka 40.

Baadhi ya ufanisi huo ni pamoja na chanjo ya malaria iliozinduliwa hivi karibuni ambayo imeifanya Kenya na mataifa mengine ya Afrika kufaidika.

Chanjo hiyo yenye wezo wa kuwalinda watu duniani kutokana na virusi hivyo ilionyesha matumaini.

Tiba hiyo inayolenga kutoa kinga dhidi ya virusi kadhaa, ilitoa kinga ya HIV katika majaribio yaliofanyiwa watu 339, kulingana na utafiti mmoja uliochapishwa katika jarida la Lancet.

Pia iliwalinda tumbili dhidi ya virusi vinavyofanana na HIV.

Majaribio zaidi tayari yamefanywa kubaini iwapo kinga iliotolewa inaweza kuwalinda watu dhidi ya maambukizi ya HIV.

Takriban watu milioni 37 duniani wanaishi na virusi vya ya HIV au Aids na kuna takriban visa vipya milioni 1.8 kila mwaka.

Lakini licha ya kupiga hatua dhidi ya HIV , tiba yake na chanjo haijapatikana.

-bbc