Chris Kirubi asimulia safari yake na saratani

KIRUBI
KIRUBI
“Saratani yangu iligunduliwa kimakosa."

Haya yalikuwa maneno ya kwanza ya mfanyibiashara Chris Kirubi akizungumzia kwa mara ya kwanza kuhusu vita vyake dhidi ya saratani. Takriban zaidi ya mwaka mmoja uliopita, Kirubi alianza siku yake kama kawaida kwa mikutano kadha wa kadha ya kibiashara kabla ya kurejea nyumbani kwake mtaani Kitusuru saa za alasiri.

Akiwa nyumbani kwake, Kirubi alianza kuhisi kibaridi na kumwita daktari wake aliyekuja na mwanapatholojia.

“Walichukuwa damu yangu na kufanya uchunguzi wa haraka na kisha wakarejea na kunieleza kwamba nilikuwa mgonjwa na nahitaji kuandamana nao hadi hospitalini. Walinikimbiza kupitia kitengo cha dharura hadi chumba cha wagonjwa mahututi katika Nairobi Hospital. Niliambiwa macho yangu yalikuwa yamebadili rangi na yalikuwa manjano na joto la mwili lilikuwa juu zaidi. Kutoka hapo uchunguzi wa kina ukaanza kwa siku chache huku wakitathmini hali yangu. Kirubi Alisema".

Aliendelea kusimulia

“Hatimaye walipomaliza, wanipa habari za kuvunja moyo kwamba nilikuwa naugua saratani katika awamu ya pili na ilikuwa inaathiri vyungo vya ndani ya mwili kama vile ini na figo. Walisema nilihitaji kwenda nje ya nchi kwa haraka ili nipate matibabu,” Kirubi mwenye umri wa miaka 78 alieleza The Star.

Kirubi kisha alisafiri Boston Marekani ambapo madaktari walimfanyia uchunguzi zaidi na kuanza matibabu.

“Hawa ni madaktari bora zaidi wa kansa na nina bahati niko hapa. Kilichofuata ni mahangaiko. Uchungu, hutotulia na wakati mwingine dawa zilikuwa na nguvu zaidi,” alisema.

Aliyekuwa afisa mkuu mtendaji wa Safaricom Bob Collymore, aliyekuwa mbunge wa Kibra Ken Okoth na aliyekuwa Gavana wa Bomet Joyce Laboso ni miongoni mwa watu mashuhuri waliofariki kutokana na saratani katika siku za hivi majuzi.

Licha ya changamoto, Kirubi hakupoteza matumaini. Aliamini Mungu na madaktari waliokuwa wakimtibu.

“Sikupoteza imani na watu walikuja kuniombea. Baada ya muda hali yangu ilianza kuimarika. Mwili wangu ulikuwa dhaifu lakini sikuwa na budi ila kuendelee na matibabu. Haikuwa rahisi,” alisema Kirubi.

Alipopata nafuu madaktari walimruhusu kurejea nyumbani na mfanyibiashara huyo mashuhuri akaabiri ndege ya kurudi Kenya ambapo amekuwa akiendelea na matibabu, na kwa sababu mwili wake hauna kinga ya kutosha kukabili magonjwa, ni wageni wachache tu wanaoruhusiwa kumttembelea.

“Imekuwa safari yenye machungu iliojaa changamoto. Nawahimiza watu wote wanaogua saratani kutopoteza matumaini. Omba lakini pia tafuta matibabu,” alisema.

“Usiruhusu kansa ifike awamu ya tatu au ya nne kwa sababu ni vigumu kwa madaktari kuitibu katika kiwango hicho,” Kirubi alisema katika wito wake.