Chuma cha Gavana Sonko ki motoni

SONKO
SONKO

Uchunguzi unaoendelea dhidi ya madai ya ufisadi yanayomhusisha Gavana wa Nairobi Mike Sonko umechukuwa mwelekeo mpya.

Hii ni baada ya ufichuzi kuonyesha kwamba baadhi ya makampuni yanayoaminka kutoa hongo ili yapewe zabuni katika City Hall yalianza kufanya biashara na gavana Sonko hata kabla ya yeye kuwa gavana.  Sonko anadaiwa kupokea shilingi milioni 20 kutoka kwa makampuni hayo na kisha yakapata zabuni ya jumla ya shilingi milioni 357 kuzoa taka katika kaunti ya Nairobi.

Katikati ya uchunguzi ni makampuni ya Toddy Civil Engineering Company Ltd na Hardi Enterprises Ltd yanayohusishwa na mfanyibiashara Antony Mwaura.  Sonko, tayari ameandikisha taarifa katika tume ya maadili na kupambana na ufisadi (EACC) na inasemekana aliambia maafisa wa uchunguzi kwamba pesa hizo zilikuwa za biashara na hazikuwa na uhusiano wowote na shughuli za kaunti.

Kampuni ya Toddy ilipewa zabuni ya shilingi milioni 424 na wizara ya maji kwa upanuzi na ukarabati wa huduma za maji katika eneo la Kwale mwezi Septemba mwaka 2018.

Inaripotiwa Sonko aliwaeleza wachunguzi kwamba mabomba ya mradi huo wa maji yalikuwa yanapita katika shamba lake ambalo kampuni ya Toddy ilichukuwa na kisha kumfidia.

Stakabadhi, zilizofikia The Star zaonyesha kuwa Toddy limted, kupitia akaunti binafsi ya Mwaura ilituma shilingi milioni moja kwa akaunti ya Sonko kama moja wapo ya malipo ya shamba la Kwale.

Sonko inasemekana aliambia maafisa wa uchunguzi kwamba pesa hizo zilitumwa kwa akaunti yake ya Equity 1132250323 - Aprili 19, 2017, na zilikuwa kwa lengo la kununua kipande cha ardhi.

EACC inataka kubaini ikiwa pesa zilizotumwa kwa akaunti ya Sonko mwaka 2017 zilikuwa na uhusiano wa kiunua mgongo ili kuchochea zabuni ya kuzoa taka iliopewa kampuni ya Hardi Enterprises inayo milikiwa na Mwaura.