Copa America: Bao la Edison Cavani lawazamisha mabingwa Chile

cavani
cavani
Bao la Edinson Cavani katika dakika ya 82 lilisaidia Uruguay kuwalaza mabingwa watetezi Chile 1-0 na kumaliza kileleni mwa kundi C la kombe la Copa America.

Chile ilimaliza ya pili na alama sita, moja nyuma ya mahasimu wao, huku Japan na Ecuador wakitoka sare ya 1-1 na kuchujwa kutoka kwa kipute hicho.

Uruguay itacheza robo fainali dhidi ya Peru huku Chile ikiminyana Equador Jumapili. Wenyeji  Brazil nao watapambana na Paraguay, huku , Argentina ikicheza na Venezuela Ijumaa.

Huko Uingereza, Steven Gerrard anasema anafahamu kua huenda Derby wanataka huduma zake lakini amejitolea kusalia na Rangers msimu ujao. Hii ni baada ya vyombo vya habari nchini Uingereza kuripoti kua Gerrard ndio chaguo la kwanza la Derby kuchukua uskani iwapo meneja wao wa sasa Frank Lampard ataondoka na kuelekea Chelsea.

The blues wamehusishwa na aliyekua kiungo wao wa kati Lampard, kufuatia kuondoka kwa Maurizio Sarri kuelekea Juventus.

Kwingineko, majadiliano ya Manchester United na Crystal Palace ya kumleta Aaron Wan-Bissaka Old Trafford yameanza upya. Palace wanaripotiwa kutaka pauni milioni 50 moja kwa moja kwa kiungo huyo wa Uingereza ambaye ana miaka mitatu iliyosalia katika mkataba wake ugani Selhurst Park.

Hata hivyo United wanaaminika kutoa ofa ya mara moja ya pauni milioni 35 na marupurupu zaidi ya jumla ya pauni milioni 15 ambayo ilikataliwa na bado hawajawasilisha ofa mpya.