Corona yabisha mlango katika kaunti ya Kisii, mhasiriwa alirejea kutoka Tanzania

ongwae
ongwae

Kisa cha kwanza cha maambukizi ya virusi ya corona kusajiliwa katika kaunti ya Kisii ni raia wa Kenya anayefanya kazi katika hoteli nchini Tanzania. Jamaa huyo alipenya mpaka na kurejea nchini wiki mbili zilizopita na kwenda katika kijiji cha Gionseri.

Gavana wa Kisii James Ongwae siku ya Jumatano alisema kwamba mhasiriwa ni mwanamume mwenye umri wa miaka 38 na tayari amehamishwa kutoka eneo la karantini katika chuo cha KMTC hadi katika Hospitali ya Rufaa ya Kisii.

Jamaa huyo alikuwa anafanya kazi katika hoteli eneo la Tarangire nchini Tanzania na Ongwae alisema yuko katika hali shwari.

Sampuli zake zilipelekwa katika kituo cha kupima virusi vya corona mjini Kisumu na kupatikana kwamba ameambukizwa. Maafisa husika wameanzisha juhudi za kusaka watu aliotangamana nao. Kufikia sasa, jamaa 14 wa familia yake wamewekwa katika karantini.

“Tumewachukulia watu wote 23 katika eneo la karantini la KMTC kama watu ambao pia alitangamana nao. Tumechukuwa sampuli zao upya na tutasalia nao katika karantini kwa siku 14 zaidi," Ongwae alisema.

"KMTC sasa litakuwa eneo la kuwatenga jamaa wote waliotangamana na mgonjwa huyo. Tumepulizia dawa chumba ambamo alikuwa akilala na katika maeneo mengine ya chuo hicho."

Gavana Ongwae aliongeza kwamba bado wanatafuta jamaa wengine watatu ambao ndio waliosalia katika orodha ya watu waliotangamana naye.

Wananchi wametakiwa kuripoti kwa mamlaka mtu yeyote anayerejea kutoka kwingineko. Kamishna wa kaunti ya Kisii Stephen Kihara ameonya kwamba kuna watu ambao wamekuwa wakitumia malori ya mizigo kuingia nchini kinyume na sheria.