Coronavirus: Madereva 4 wa malori kutoka Tanzania wapatikana na virusi hivyo Uganda

UGANDA
UGANDA
Wizara ya afya nchini Uganda imetangaza wagonjwa wanne wapya wa virusi vya corona na kufanya idadi ya wanaothirika na ugonjwa huo kufikia 79.

Wagonjwa hao wanne ni madereva wa malori kutoka Tanzania waliowasili nchini humo kupitia mpaka wa Mutukula.

Wagonjwa hao ni miongoni mwa sampuli 1, 578 zilizochukuliwa kutoka kwa madereva wa malori.

Kati ya sampuli za wakaazi 411 zilizochukulia ili kufanyiwa vipimo hakuna hata mtu mmoja aliyekutwa na ugonjwa huo.

Hatua hiyo inajiri siku chache tu baada ya Uganda kuwarudisha nyumbani kwa lazima raia mmoja wa Tanzania na mwingine wa Kenya ambao walikutwa na virusi hivyo.

Uamuzi huo umedaiwa kuathiri uhusiano kati ya mataifa hayo wanachama wa Afrika mashariki na hivyo basi kuhatarisha usafirishaji wa mizigo kati yao.

Kufurushwa huko ambako ni kinyume na mwongozo wa shirika la Afya duniani WHO kuhusu jinsi ya kukabiliana na majanga kama vile Covid-19 pia, umeliweka katika ratili soko huru la Afrika mashariki.

Uganda imedaiwa kuwarudisha nyumbani kwa lazima madereva hao wa malori ambao walikutwa na virusi vya corona huku jopo lililoundwa nchini Sudan Kusini kukabiliana na Covid-19 likiamua kuwafurusha Wakenya wawili kwa kutumia ndege kulingana na gazeti la The East African .

Dereva mwanamume mwenye umri wa miaka 27 alikutwa na virusi hivyo kati ya madereva 372.

Sampuli yake ilichukuliwa katika kituo cha kibiashara kilichopo mpakani cha Malaba na anatarajiwa kurudishwa nyumbani ili kupatiwa matibabu.

Huku takriban malori 1, 000 ya mizigo yakidaiwa kuingia katika taifa hilo kwa siku, Madareva wa malori ya masafa marefu wamekuwa na wasiwasi mkubwa nchini Uganda baada ya kuthibitishwa kuwa chanzo kikuu cha ugonja huo miongoni mwa raia wa kigeni.

Kati ya visa vipya vya Covid vilivyotangazwa nchini Uganda siku ya Ijumaa, wagonjwa sita walikuwa madereva wa malori kutoka Tanzania waliowasili kupitia mpaka wa Mutukula huku madereva wengine watano wakidaiwa kutoka Kenya waliongia kupitia mpaka wa Malaba na Busia.

Idara ya Afya nchini Uganda inayosaidiwa na vikosi vya usalama imedaiwa kumsaka dereva wa lori wa Tanzania ili kumrudisha nyumbani kwa matibabu.

Tukio lingine ni la dereva mwingine wa malori raia wa Tanzania mwenye umri wa miaka 34 kutoka Dar es Salaam ambaye aliwasili katika mpaka wa Mutukula tarehe 16 Aprili na ambaye hakuonyesha dalili zozote za Covid-19.

Kenya imekuwa ikiwatibu baadhi ya raia wa kigeni wanaokutwa na virusi hivyo kulingana na kaimu mkurugenzi wa huduma ya afya Dkt Patrick Amoth.

''Tumewatibu wagonjwa wengi wa mataifa ya kigeni kutoka Cameroon, Pakistan, Burundi na DRC. Kama taifa hatujaona sababu ya kuwatimua kutokana na hatari zinazohusishwa na usafiri wakati mtu anapougua virusi hivyo'', alisema Dkt. Amoth.

''Inashangaza mtu kufanya uamuzi kama huo kwa sababu unaweza kuwaambukiza watu wengi zaidi unapomruhusu muathiriwa wa virusi vya corona kusafiri mbali wakati ambapo ingekuwa bora kumtibu katika taifa alilokutwa na virusi hivyo''. Aliongezea.