COVID 19 : Brazil ni nchi ya pili iliyopitisha vifo 50,000

Brazil imekuwa nchi ya pili, baada ya Marekani, kuandikisha zaidi ya vifo 50,000 kutokana na virusi vya Corona.

Wizara ya Afya nchini humo inasema jana pekee, wagonjwa 641 walifariki, huku viwango vya maambukizi ya ugonjwa huo vikiongezeka hadi milioni moja kufikia wikendi.

Wataalamu wameonya kuwa kilele cha maambukizi nchini Brazil bado hakijafikiwa.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limerekodi ongezeko kubwa zaidi la maambukizi ya ugonjwa huo kwa siku, huku Amerika kusini ikiwa na idadi ya juu zaidi ya maambukizi mapya.

Kati ya visa vipya 183,000 vya maambukizi yaliyoripotiwa katika kipindi cha saa 24, zaidi ya asilimia 60 ni kutokea Kaskazini na Kusini mwa America, shirika hilo lilisema.

Licha ya kuongezeko kwa mlipuko wa virusi, maelfu ya wafuasi wa rais wa Brazil Jair Bolsonaro wameshiriki maandamano sambamba na mahasimu wao siku ya Jumapili

Maandamano dhidi ya serikali yanashinikiza Bwana Bolsonaro aondolewe madarakani.

Wafuasi wake wanasema Bunge la Congress na mahakama ya juu zaidi inajaribu kudhibiti uwezo wake.

Rais Bolsonaro amekosolewa vikali kutokana na jinsi anavyoshughulikia mlipuko wa virusi vya corona nchini humo.

Amepinga hatua ya kuweka amri ya kutotoka nje na kutofautiana hadharani na ushauri wa wizara yake ya afya.

Siku ya Jumapili, wizara hiyo ilitangaza vifo zaidi ya 641 vilivyorekodiwa katika kipindi cha saa 24 na kufikisha 50,617.

Pia nchi hiyo ilithibitisha maambukizi mapya zaidi ya 17,000 katika kipindi sawia na hicho.

Ni Marekani pekee iliyo na idadi ya juu zaidi ya maambukizi, ikiwa na jumla ya watu milioni 2.2 walioambukizwa huku watu 120,000 wakifariki.

Bw. Bolsonaro anadai kuwa athari za kiuchumi zitakuwa mbaya zaidi kuliko maambukizi ya virusi vyenyewe, hoja ambayo inaungwa mkono na wengi. Lakini hatua yake imesababisha mawaziri wawili wa Afya kujiuzulu.