Covid 19:Kenya yasajili kisa cha 4 cha virusi vya Corona

Kenya imesajili kisa chake cha nne cha virusi vya Corona. Waziri wa afya Mutahi Kagwe amesema mtu wa nne aliyesafiri kutoka London ndiye aliyepatikana na virusi vya ugonjwa huo na ametengwa katika wadi maaluma kwa uangalizi.

Kisa cha kwanza cha virusi hivyo kiliripotiwa nchini  siku ya Ijumaa wiki jana na visa vingine viwili kuthibitishwa siku ya Jumapili. Kagwe pia amewahimiza wahudumu wa matatu kuhakikisha kwamba hali ya usafi inadumishwa katika vituo vya magari. Wakenya pia wameshauriwa kuepuka maeneo yenye watu wengi.

Kagwe pia amesema Kenya itaendelea kupokea mizigo inayoingia nchini kutoka China. Wahudumu wa ndege na meli za mizigo hata hivyo watatakiwa kujitenga kwa muda baada ya kuwasilai nchini. Kagwe amesema hatua hiyo inalenga kuzuia kuzorota kabisa kwa uchumi wa taifa. Tayari viwanda kadhaa nchini Uchina  vimerejelea oparesheni.

Waziri pia amethibitisha kuwa watu 23 waliokuwa wamewekwa katika uangalizi baada ya kukaribiana na mgonjwa wa kwanza wameruhusiwa kwenda nyumbani baada ya kupatikana bila virusi.