David kakake Ruto, asimulia jinsi maisha yalivyokuwa magumu wakiwa wadogo

Wakiwa na umri mdogo, David ambaye ni kakake naibu wa rais William Ruto anasema iliwabidi kutembea bila viatu kwa umbali kilomita nne hadi shuleni kutokana na hali yao ya umaskini.

David Ruto anasema kuwa shule yake ilikuwa mbali, lakini alililazimika kutembea huku nyasi, mawe na ardhi mkavu yakimpa maumivu tele miguuni.

Kulingana naye, familia yao haingeweza kumudu gharama ya mavazi kwa kuwa tayari ilikuwa na mzigo mzito wa kugharamia vyakula na mahitaji mengine muhimu.

"Tulikuwa maskini. mimi pamoja na ndugu zangu tulitembea zaidi ya kilomita nne kila siku kwa miguu tukienda shule," David anasimulia.

Aidha anasema kwamba kutokana na kukosa viatu, vidole vyao vilikuwa vinaumia sana kutokana na jua kali, mawe, funza pamoja na matope wakati wa mvua.

"Hakukuwa na barabara katika kijiji chetu. Nililelewa eneo la Uasin Gishu...Ni eneo lililokuwa limesahaulika kutokana na maendeleo," alisema.

Safari ya David kuibuka kuwa mfanyakazi maarufu, kupata shahada ya uzamifu kutoka chuo kikuu cha Capella Marekani, na hata kutambulika kuwa mfawidhi mkubwa yalianza kwenye lindi la uchochole.

Kwa sasa anazuru maeneo mengi ya nchi, huku akitambua na matatizo yanayowakumba wakaazi na kuwaunganisha na maafisa wa serikali husika.

"Sifanyi kazi na serikali. Lakini mimi ni kutuma ujumbe. Ninazuru maeneo yote nchini bila kubagua. Ninashuhudia matatizo wanayopitia wananchi na kuwashilisha kwa mbunge husika ili kupata suluhu," alisema.

Alisema kwamba lengo lake ni kuhakikisha kuwa  huduma za kiserikali na maendeleo yanafikia wananchi wote  bila ubaguzi wa kimaeneo.