David Maraga atofautiana na mabadiliko maalum ya rais Uhuru

Jaji Mkuu David Maraga, ametoa maoni yake kuhusiana na maagizo maalum ya Rais Uhuru kuvunja taasisi ya rais ambayo ilifanya mabadiliko katika serikali.

Katika taarifa mnamo Alhamisi Juni 4, Maraga alisema mabadiliko hayo hayawezi kutekelezwa katika idara ya Mahakama kwani taasisi zote ni tofauti.

Jaji Mkuu David Maraga alisema mabadiliko hayo hayawezi kutekelezwa katika Idara ya Mahakama kwani taasisi zote ni tofauti.

Maraga alikosoa mabadiliko hayo maalum ambayo yameweka Idara ya Mahakama chini ya Serikali Kuu. "Taasisi hiyo haiwezi kusimamia huduma za idara nyingine tofauti na tume zingine zinazojisimamia.

Serikali kuu haiwezi kubadilisha ama kutoa mwelekeo kwa Idara ya mahakama ama kwa Jaji Mkuu," alisema Maraga katika taarifa hiyo.

Jaji huyo Mkuu aliomba Ofisi ya Rais kubainisha bayana mabadiliko hayo mapya kwa umma huku akidai kwamba huenda kulikuwepo na makosa.

"Huku ikiwa agizo maalum haijaanza kutekelezwa kisheria, katiba yaelezea vyema kuhusu kubuniwa kwa Idara ya mahakama na Tume ya Huduma za Mahakama na mamlaka yao, ni vyema umma kuelewa kwa demokrasia ya katiba," Amesema Maraga

"Kwa hivyo ni wazi kwamba Agizo hilo ni la kutekelezwa katika idara za Serikali Kuu, ninataka kuamini kuwa kulikuwepo na makosa na Ofisi ya Rais itarekebisha makosa hayo," aliongezea Maraga.

Haya yanakujia baada ya Rais Uhuru mnamo Jumatano Juni 3, alitia saini agizo maalum na kufutilia mbali taasisi ya rais maarufu kama 'presidency'.

Maana ya hatua hiyo ni kuwa sasa naibu rais hatakuwa na mamlaka yake kando kama vile uajiri wa wafanyikazi wake.

Jukumu hilo sasa litachukuliwa na afisi ya rais sawa na bajeti zingine zilizokuwa zikitengewa afisi yake chini ya mpango wa awali.