David Rudisha ahusika katika ajali ya barabarani

Bingwa wa riadha duniani David Rudisha siku ya Jumapili alikimbizwa katika hospitali mjini Nairobi kwa matibabu zaidi baada ya kuhusika katika ajali ya barabarani eneo la Kijauri, Borabu, Kaunti ya Nyamira.

Kakake Shadrick Rudisha aliambia The Star kupitia simu kwamba, walikuwa njiani kuja Nairobi ili afanyiwe uchunguzi zaidi kubaini kama alipata majeraha yoyote ya ndani wakati gari lake lilipogongana ana kwa ana na basi la Ena Coach lililokuwa likielekea Nairobi kutoka Kisii.

Rudisha alikuwa anaelekea nyumbani kwao kutoka Nairobi, Shadrick alisema.

Afisa mkuu wa polisi wa Keroka Walter Opondo aliambia The Star kwamba hapakuwepo majeruhi kwenye basi.

Alisema Rudisha kwanza alikimbizwa katika hospitali ya Gucha mjini Keroka alikotibiwa kwa majeraha madogo kabla ya kuruhusiwa kwenda nyumbani.

" Alitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani," Opondo alisema.