Deal Breakers: Kuanzia kuficha kwamba una mtoto hadi kugunduliwa kwamba uliolewa zaidi ya mara 2. Haya hapa mambo ya kuepuka katika uhusiano mpya

marriage breaker
marriage breaker
Wakati wa kuanza uhusiano na mtu, kuna mengi ambayo watu huficha kwa lengo la kujiuza kama watu tofauti ama walio bora.

Lakini ni vyema endapo utakuwa mkweli kuanzia mwanzo kwani visa ni vingi vya walioifanya feki na kuepuka kusema ukweli kisha baadaye wakalipia gharama kubwa ya uhusiano wao kuvunjika.  Soma kuhusu baadhi ya vitu ambavyo huharibu uhusiano mzuri hata iwapo mnapendana .

Kutosema una mtoto

Akina dada ndio waathiriwa wakubwa wa mtego huu. Iwapo unampenda mwenzio na unaamini kwamba atakupenda  pamoja na  mzigo wako basi ni vyema kumuambia tangia mwanzo kwamba una mtoto au watoto katika uhusiano wako wa awali. Kuna wengi ambao huficha wanao na kisha baadaye baada ya hata kuingia katika ndoa, mwenzio anagundua kwamba ulimhadaa. Hili huvuruga sana uaminifu kati yenu na hakuna uhusiano unaoweza kuboreka bila kuaminiana.  Wanaume pia huwaficha wanadada kwamba hawana mtoto ama watoto na hilo baadaye huleta matatizo mengi. Ilimradi mwenzako yuko tayari kukupenda hata ukiwa na mwanao basi unafaa kuwa mkweli kwa kufichua hilo. Endapo  unayekutana naye atapata ugumu wa kukupenda anapojua kwamba una mtoto ama watoto basi huyo hakuwa wako wala hakufai.

Umewahi kuoa/Kuolewa?

Kuna watu wenye ustaarabu ambao watakuambia mnapoanza uhusiano kwamba  walikuwa katika ndoa hapo awali na mambo hayakuwaendea vizuri. Hilo jambo ambalo mpenzi wako mpya nafaa kujua ili pia akusaidie kujiboresha na kuepuka masaibu  uliyopitia katika ndoa yako iliyofeli. Usiogope kusema wazi kwamba uliwahi kuoa au kuolewa na hata umuambie mwenzako mbona ndoa yako ama uhusiano wako uliotanguliwa haukudumu. Hili litawasaidia kuboreka katika uhusiano wenu mpya. Inazua mtafaruku mkubwa endapo mwenzako atagudua baadaye kupitia watu wengine kwamba uliwahi kuwa katika ndoa na hujawahi kumueleza. Atahisi kudanganywa na atashangaa ni mambo gani mengine kujihusu hujamuambia.

Kujibadilisha tabia au mtazamo

Ni jambo linalojulikana kwamba unapokutana na mtu mgeni katika uhusiano, utajaribu kadri ya uwezo wako kutoa taswira ya uzuri ili kumvutia. Walakini kuna miaka ya kufanya hilo. Usije ukafanya kila jambo feki ili kujitambulisha kama mtu usiweza kumuiga maisha yote. Wanawake wana tabia hiyo sana na utasikia kuhusu mtu alivyobadilisha namna anavyozungumza, kutembea na hata   anachokula. Utasikia kuhusu wasichana watakaokuambia kwamba hawajawahi kula ‘githeri’ tangu walipozaliwa kumbe wamebugia mlo huo maisha yao yote. Baki jinsi ulivyo ili mwenzako akupende vivyo hivyo. Usimuuzie mwenzako mhusika wa filamu kwani wakati utakapofika urudi kuwa wewe atafikiri umebadilika.  Licha ya kuwepo na hatari ya kuachwa, ukweli unasalia kuwa ngao thabiti ya kudumisha uhusiano au ndoa.