Dennis Itumbi kuachiliwa chini ya masharti

Hakimu wa mahakama ya juu alimpa Dennis Itumbi masharti manne ambayo lazima ayafuate akiwa huru.

Dennis aliamrishwa kuripoti kwa kituo cha polisi cha Muthaiga kila siku mbili na kupeleka pasipoti yake mahakamani.

Jaji pia alisema kuwa Dennis atarudishiwa power bank yake siku ya Jumatano, Julai 10 lakini simu yake itabaki kizuizini kwa muda wa siku 14.

Dennis pia alikatazwa kutoa maoni yote kuhusu kesi hiyo kwa vyombo vya habari vya kijamii au vya kawaida.

Kesi yake itaskika tena mwezi wa Julai tarehe 22.

Mwendesha mashtaka alikuwa ameomba mahakama kuzuia mshtakiwa siku zingine tisa.

Itumbi aliripotiwa na kufungwa kwa sababu ya barua bandia iliyokuwa na mpango wa kumwua Naibu Rais William Ruto.

Mnamo Julai 4, Itumbi alihukumiwa kuzuiliwa na polisi kwa muda wa siku tano ili kuruhusu uchunguzi kuendelea.