'Dosi yangu ya heroini kila asubuhi hugharimu shilingi 400' - Lisa

Heroine
Heroine
"Maumivu ya kuacha ni kama mwanamke mwenye hedhi kali au gesi ikiambatana na kudungwa visu tumboni.'

Hayo ndiyo masaibu yanayomkumba kila uchao Lisa Marete mwenye uraibu wa mihadarati ya heroini

Kila siku anapoamka, fikra na hamu ya Lisa huwa ni kupata dosi ili akili yake hufunguke!

Anahitaji misokoto miwili ya gramu 0.1 kila asubuhi ili akili yake ifanye kazi vizuri. Dosi yake inagharimu shilingi 400.

Bila kuwa na heroini anasema kwamba hali yake huwa si shwari, anatokwa na jasho jingi, kuhisi kutapika, kuchanganyikiwa pamoja na maumivu makali.

Hapo ndipo hana budi kusaka mwuuzaji ambaye ni jirani wake katika vitongoji duni vya Mathare.

Lisa amepitia hayo zaidi ya mara mia.

Akiwa na uraibu huu kwa zaidi ya miaka 20, kwa sasa ana umri wa miaka 43 na ana hamu na ghamu ya kumaliza kiu yake... akili yake inmwongoza kwenye huo 'unga.'

Uraibu wa heroini ni uzoelevu ulio ghali sana. "Dosi yangu ya kila asubuhi ugharimu shilingi 400. Wanaume hunilipa kiasi kidogo cha shilingi 50 nikilala nao," alisema.

Ili kukata kiu yake, Lisa hulazimika kufanya mapenzi na zaidi ya wanaume 10 ili kupata pesa za dosi yake.

Hata ingawa yeye hutumia dawa aina ya Methadone ambayo huwa ni vibadala vya kuzuia hamu ya heroini, lisa anasema kwamba yeye hutaka  'unga' wenyewe.

Anapitia maisha magumu akijaribu kurudi katika maisha yake ya kawaida, akipigana na pombe, kuvuta heroini na kwa sasa anajidungia dawa hizo za kulevya.

Tulimtazama akijidungia dawa hizo na kustahimili uchungu wa sindano. Mwanzo alichoma unga huo hadi ukawa likwidi.

Kisha akachaza kwenye sindano, akafunga mkono wake ili mishipa ionekane, kisha heroini ikaingia kwenye damu na baada ya dakika tano, alikuwa kwenye dunia yake.

Anasema kwamba dawa hii ya kulevya inapokuwa 'nzuri', yeye hujikuna kwenye sehemu zake za siri au kichwani chake.

Mnamo 2018, tume ya Nacada ilisema kwamba watu 162,863 wanajulikana kutumia marijuana huku wengine26,058 wakisemekana kutumia heroini.