DPP aagiza DCI na IPOA kuchunguza madai ya polisi kumdhulumu MCA Nairobi

DPP LETTER
DPP LETTER
Mkurugenzi wa mashtaka ya umma Noordin Haji ameagiza idara ya DCI na mamlaka huru ya shughuli za polisi (IPOA) kuanzisha uchunguzi kuhusiana na madai ya kushambuliwa kwa mwakilishi wadi wa Mlango Kubwa Patricia Mutheu.

katika barua yake Haji alisema kwamba hatua hii iliafikiwa baada ya mashauriano ya kina baina yake na Inpekta mkuu wa polisi Hillary Mutyambai.

Soma habari zaidi;

DPP alisema kwamba Inspekta mkuu wa polisi amemhakikishua kuwa uchunguzi wa madai hayo tayari umeanza.

Ametaka DCI na IPOA kuwasilisha ripoti ya uchunguzi kwa afisi yake punde tu watakapokamilisha zoezi hilo.

Mamlaka huru ya shughuli za polisi (IPOA) ilikuwa tayari imethibitisha kuanzisha uchunguzi kuhusiana na tukio hilo lililotokea katika City Hall mjini Nairobi siku ya Jumanne.

Soma habari zaidi;

Mwenyekiti wa IPOA Anne Makori siku ya Jumanne alisema kwamba mamlaka hiyo iliwasiliana na watu waliokuwepo wakati wa ghasia zilizoshuhudiwa katika bunge la kaunti ya Nairobi mapema siku ya Jumanne.

“Uchunguzi huu wa awali unalenga kubainisha hatua ya polisi waliotumwa kushika doria ghasia zilipozuka na ambapo kesi moja ya kujeruhiwa kwa mwakilishi mmoja wa wadi iliripotiwa,” Makori alisema.

Makori aliongeza kuwa watahakikisha kwamba polisi hawatumii nguvu kupita kiasi kila wanapotuliza ghasia na kwamba tukio lolote ambapo polisi wanatumia nguvu kupita kiasi na kinyume na sheria hatua kali zitachukuliwa dhidi ya maafisa husika.

Soma habari zaidi;

Ghasia zilizuka katika makao makuu ya kaunti ya Nairobi baada ya kundi moja la wakilishi wadi kujaribu kumpokeza Spika Beatrice Elachi notisi ya hoja ya kutaka kumfurusha.

Mutheu alisema kwamba alitandikwa na polisi alipokaidi amri ya kuondoka wakati wa ghasia hizo.