DPP aagiza kukamatwa kwa waziri wa fedha Henry Rotich

haji
haji
Chuma cha waziri wa fedha Henry Rotich ki motoni baada ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma Noordin Haji kuagiza kukamatwa kwake pamoja na katibu wa kudumu wa fedha Kamau Thugge na maafisa wengine wa ngazi za juu katika serikali kuhusiana na sakata ya mabwawa ya Kimwerer na Arror.

Noordin alisema siku ya Jumatatu kwamba maafisa wakuu katika serikali walikiuka kanuni za utoaji zabuni katika sakata ya mabwawa hayo.

"Kanuni nyingi za utoaji zabuni zilikiukwa na kukwepwa ili kuhakikisha kwamba kampuni ya CMC di Ravenna inapata kandarasi ya kujenga mabwawa hayo," Haji alisema.

Hii ni licha ya kampuni ya CMC di Ravenna kukumbwa na matatizo nchini mwao Italy.

Haji na mwenzake katika idara ya DCI George Kinoti walisafiri nchini Italy Juni 10 kukamilisha uchunguzi wao kuhusu sakata ya mabwawa ya Kimwerer na Arror.

Wawili hao walikutana na wenzao mjini Turin kujadili sakata hiyo ya mabilioni ya pesa.

DCI alikuwa anachunguza uwezekano wa kupotea kwa shilingi bilioni 21 zilizonuwiwa kwa ujenzi wa mabwawa mawili katika eneo la Kerio Valley.

Alianza uchunguzi wake mwezi Disemba mwaka jana na kwasababu ya uzito wa na ugumu wa kesi hiyo, alikuwa ameitisha msaada kutoka kwa idara zingine za serikali ikiwemo idara ya kitaifa ya ujasusi NIS.