ELDORET: Mwanamke auawa, vipande vya mwili vyachukuliwa

Polisi wanachunguza kisa kimoja ambacho mwanamke aliuawa na vipande vya mwili wake kuchukuliwa katika eneo la Moi Bridge, liliko kwenye mpaka wa kaunti za Trans Nzoia na Uasin Gishu.

Miguu yake miwili na mkono mmoja haikupatikana baada ya mwanamke huyo kupatikana akiwa ameuawa kinyama. Polisi wanakisia mauaji hayo yasiyo ya kawaida yalitekelezwa na jamaa anayeshukiwa kuwa mpenzi wa mwendazake.

Ben Kibe ambaye ni jirani yake mwanamke huyo, alisema kuwa marehemu alikuwa nyumbani kwake pekee yake wakati kisa hicho kilitendeka.

Mwili wake ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Kitale County Referral, huku polisi wakiendeleza uchunguzi wao kuhusu kisa kilichowaacha wenyeji wa Moi's Bridge na mshtuko mkuu.

Hayo yakijiri, wabunge wa ukanda wa pwani wameshauriwa kutengea elimu mgao wa kutosha wa basari kutoka kwa hazina ya kitaifa ya CDF, ili kuhakikisha wanafunzi wote kutoka kwa familia zisizojiweza eneo hilo wamesoma. 
 
Mbunge wa Mwatate Andrew Mwadime anasema hatua hiyo itasaidia kuinua viwango vya elimu ambavyo vimedorora eneo la Pwani kutokana na umasikini miongoni mwa wazazi. 

-Solomon Muingi