Fikra za kishenzi! Waliotimuka mbio baada ya kupatikana na Corona watafutwa na polisi Mombasa

7bfK5OJG
7bfK5OJG
NA NICKSON TOSI

Maafisa wa usalama kaunti ya Mombasa sasa wameanzisha msako mkali dhidi ya watu watano waliotimuka mbio baada ya kufahamishwa kuwa walikuwa na virusi hivyo hatari katika mtaa wa Kale ama Old Town.'

Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho alisema jamaa hao watano walitimuka na jamaa zao wa  karibu baada ya kufahamishwa taarifa hiyo na maafisa wa afya waliokuwa wanaendeleza shughuli za kuwapima wakaazi wa Old Town.

Hapa Old Town, kati ya watu 65, watano wametoroka na familia zao wameenda kujificha. Sasa wameweka maisha ya familia yao katika hali hatari,” alisema  Joho.

Kisa hicho kimejiri siku chache tu baada ya wakaazi hao kuwafurusha maafisa wa afya waliokuwa wametumwa na serikali kuwapima.

Mji wa Old Town Mombasa umekuwa ukiangaziwa zaidi na serikali baada ya visa vingi vya maambukizi kuripotiwa katika eneo hilo.

Kutokana na tukio hilo, polisi sasa wameanzisha msako mkali dhidi ya watu hao watano.

Mtaa wa Old Town Mombasa na Eastleigh jijini Nairobi yote imefungwa kutokana na idadi kubwa ya maambukizi ambayo yanashuhudiwa.