Flagbearer: Mariga kupeperusha bendera ya Jubilee Kibra

McDonald Mariga aliyeteuliwa kuwa mgombeaji wa chama cha Jubilee
McDonald Mariga aliyeteuliwa kuwa mgombeaji wa chama cha Jubilee
  Aliyekuwa mchezaji wa  timu ya taifa ya Harambe  Stars McDonald Mariga  ametangazwa kuwa mgombeaji wa chama cha Jubilee katika uchaguzi mdogo wa Kibra . Mwenyekiti wa bodi ya uchaguzi ya chama cha Jubilee Andrew Musangi  amesema Mariga ndiye mgombeaji mwenye  sifa tosha na uhusiano wa karibu na wakaazi  wa Kibra .Mariga  alikuwa katika makao makuu ya chama cha Jubilee siku ya jumatatu  ili kuhojiwa na bodi ya uchaguzi  na Musangi alitangaza baadaye kwamba ‘Mariga ndiye atakayekuwa sauti ya Jubilee katika eneo bunge la Kibra’. Baadhi ya  masuala mabyo Mariga aliulizwa maswali kuyahusu na chama cha Jubilee ni   kuhusu sera za chama hicho ,  iwapo anaelewa kazi ya ubunge  , uwezo wa kufadhili kampeini  na  mpango wake wa wakaazi wa Kibra .

Bodi ya kitaifa ya Uchaguzi  pia iliwahoji wagombeaji kuhusu ufahamu wa manifesto ya Jubilee  na uwezo wa kuafikia  maazimio yake . Jumla ya wagombeaji 16 walitaka kupewa  tiketi ya chama cha Jubilee . Miongoni mwa wagombeaji hao ni  Morris Peter Kinyanjui, Walter Trenk, Said Ibrahim na  Doreen Wasike.Mariga  sasa atamenyana na wagombeaji kutoka vyama vya ODM ,ANC na Ford Kenya katika uchaguzi huo mdogo wa  Novemba tarehe 7.ODM inatarajiwa  kufanya uchaguzi wake wa mchujo  siku ya jumamosi  baada ya  kuahirisha zoezi hilo kwa ajili ya ukosefu wa usalama  kwa ajili maafisa wengi wa idara za ulinzi walikuwa wakijishughulisha na  sensa .ANC  ilimtangaza  Eliud Owalo  kama mgombeaji  wake kwa uchaguzi huo mdogo .  Muda wa kampeini za uchaguzi huo mdogo utaanza septemba Tarehe 9 hadi Novemba  tarehe 4 . Kiti hicho  cha Kibra kiliachwa wazi baada ya kifo cha  Ken Okoth  tarehe 26 Julai mwaka huu kwa ajili ya ugonjwa Saratani .