Ligi za mbali mbali za soka duniani zinarejea wikendi hii baada ya
mapumziko ya kimataifa wikendi iliyopita kupisha mechi za kufuzu makombe mbali
mbali ya mabara duniani.
Ligi kuu Uingereza inarejea kwa mechi za raundi ya nane ya
msimu huu, zitakazochezwa Jumamosi, Jumapili na Jumatatu.
Jumamosi 19, Tottenham itacheza dhidi ya West Ham mechi ya
mapema mwendo wa saa 8 na nusu.
Jumla ya mechi tano zitachewa Jumamosi mwendo wa saa 11
ambapo Man United itakuwa nyumbani kumenyana na Brentford wakati Fulham itaialika
Aston Villa. Everton itakuwa ugenini kucheza dhidi ya Ipswich Town wakati Newcastle
na Southampton wakiwakaribisha Brighton na Leicester mtawalia wakati sawia.
Mikel Arteta na wachezaji wake watasafiri kuelekea uwanja wa
Vitality ambapo watacheza dhidi ya mwenyeji wao Bournemouth saa moja na nusu
jioni.
Jumapili, itakuwa zamu ya mabingwa watetezi Manchester City
wakilenga kuendeleza msururu wa matokeo bora watakapocheza na Wolves saa kumi
jioni kabla ya mechi inayosubiriwa zaidi wikendi hii kati ya Liverpool na
Chelsea kuchezwa saa kumi na mbili Jumapili hiyo.
Aidha raundi ya nane ya msimu 2024/2025 itakamilika siku ya
Jumatatu ambapo Nottingham Forest watakuwa nyumbani mwendo wa saa nne usiku
kucheza dhidi ya Crystal Palace.
Ligi inaporejea, Liverpool inaongoza jedwali kwa alama kumi
na nane, wakifuatiwa na Man City kwa alama kumi na saba. Nafasi ya tatu
inashikiliwa na Arsenal kwa alama sawa na Man City, Chelsea ikitulia katika
nafasi ya nne kumi na nne wakitoshana na Aston Villa wanaoshikilia nafasi ya
tano kwa uchache wa magoli.
Manchester United inasuasua katika ukurasa wa pili wa jedwali la EPL wakiwakatika nafasi ya kumi na nne kwa alama nane baada ya mechi saba za msimu wa 2024/2025.
Nchini Uhispania, La Liga itaingia raundi ya kumi mechi
zikiratibiwa kuchezwa kuanzia Ijumaa hadi Jumatatu.
Girona watacheza dhidi ya Real Sociedad Jumamosi saa kumi na
nusu kisha saa nne usiku Celta Virgo kucheza dhidi ya Real Madrid. Barcelona
watakuwa nyumbani kucheza dhidi ya Sevilla mwendo wa saa nne usiku.
Kwenye Bundesliga, Borussia Dortmund watacheza saa tatu na
nusu Ijumaa usiku dhidi ya FC St. Pauli. Bayer Leverkusen watawaalika Eintracht
Frankfurt saa kumi na nusu jioni wakati huo, RB Leipzig wakimenyana ugenini na
Mainz nao Bayern Munich wakipambana na VfB Stuttgart.
Ligi ya Bundesliga inaingia raundi ya saba.