Gavana Sonko apelekwa hospitalini KNH kwa matibabu ya dharura

Gavana wa Nairobi Mike Sonko amepelekwa katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta kwa matibabu ya dharura.

Mkurugenzi mkuu wa mawasiliano wa Sonko Elkana Jacob amethibitisha kuwa gavana alipelekwa hospitalini Jumatatu 9.45 usiku kutoka gereza la Kamiti Maximum alipopelekwa baada ya kesi yake kusikizwa mahakamani Milimani.

Sonko anasemekana kulalamikia maumivu kifuani tangu Ijumaa alipokamatwa akiwa Voi.

Jaji anayeshughulika na kesi za ufisadi Douglas Ogoti alisema kuwa gavana Sonko ana uhuru wa kupata matibabu akiwa rumande.

Wakili Cecil Miller anayewakilisha Sonko kortini alisema kuwa gavana anahitaji uchunguzi wa kimatibabu wa CT scan na tayari ameshapewa  dawa za kutuliza maumivu.

Aliongeza kusema kuwa Sonko huenda anaweza kuwa alivunjwa mbavu zake alipokuwa akikamatwa.

Mwendesha mashtaka hakupinga maafisa wengine waliokamatwa na Sonko kuachiliwa kwa dhamani huku akisihi mahakama kuzingitia kiwango pesa wanachodaiwa kutumia vibaya.

Aidha Ogoti aliagiza Sonko kupewa matibabu chini ya ulinzi wa maafisa wa gereza.