Ghasia Mombasa huku polisi wakitawanya waandamanaji

Maafisa wa polisi walilazimika kutumia vitoa machozi kuwatawanya wanaharakati wa haki za kibinadamu na wahudumu wa malori ya kusafirisha mizigo waliokuwa wakiandamana kupinga agizo lililositishwa kwa muda kutaka shehena zote kutoka bandari ya Mombasa zisafirishwe kwa SGR.

Mwanaharakatiwa shirika la Muhuri Francis Auma, Hussein Khalid wa Haki Africa na viongozi wa muungano wa wafanyibiashara wa kanda ya Afrika mashariki ni miongoni mwa watu 20 waliokamatwa. Watu kadhaa waliokuwa wakishiriki maandamano hayo pia walijeruhiwa wakati wa makabiliano hayo.

Maandamano hayo ya kila wiki kupinga agizo hilo la Mamlaka ya ukusanyaji ushuru nchini (KRA) yamekuwa yakifanyika kila Jumatatu. Yamekuwa yakifanyika kwa njia ya amani lakini leo yakiwa maandamano ya nne yameshuHUdia ghasia baada ya polisi kuamua kuyatawanya.

Mbunge wa Kisauni Ali Mbogo alikuwa ametawaka wanaharakati hao kusitisha maandamano hayo kwa sababu viongozi wa Pwani walikuwa tayari wamepanga kukutana na rais Uhuru Kenyatta kujadili swala hilo kwa kina.

Hata hivyo wazo la mbunge huyo halikufurahisha waandalizi wa maandamano hayo na wakamkaripia sana mbunge huyo aliyekuwa ameandamana na seneta Mohamed Faki wa Mombasa wakiwashtumu kwa kuunga serikali mkono kuwanyanyasa.

Afisa wa masawasiliano wa shirika la Muhuri Cornel Oduor alisema ilikuwa makosa kwa polisi kuwatawanya na ilhali walikuwa wamefuata kanuni zote kisheria kupata idhini ya kuandamana.