Gor Mahia imetozwa faini kutokana na tabia ya mashabiki wake

Gor Mahia imetozwa faini ya shilingi elfu 750 na kamati ya nishamu ya CAF kutokana na tabia ya mashabiki wake wakati wa mechi yao ya CAF confederation dhidi ya Motema Pembe ya DR Congo uwanjani Kasarani.

Wakati wa mechi hiyo mashabiki wa Gor Mahia walitupa makombora uwanjani, jambo ambalo ni kinyume cha kanuni za CAF. Gor Mahia wana siku tatu kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo na siku 60 kulipa faini hiyo.

Hii ni mara ya pili klabu hio imetozwa faini na Caf mwaka huu kutokana na tabia ya mashabiki wake.

Sony Sugar ina masaa 48 kueleza kilichowapelekea kutocheza mechi yao na Zoo Kericho jana. Sony huenda wakashushwa daraja iwapo hawatajieleza kwa KPL.

Sony Sugar imeshawahi kukosa kujitokeza kwa mechi ya KPL dhidi ya Tusker na AFC Leopards. Kulingana na kanuni za KPL klabu yoyote inayokosa kuheshimu mechi tatu itashushwa daraja. Chemelil Sugar pia ilikosa kucheza mechi yake dhidi ya KCB. Vilabu hivyo viwili vimekua na matatizo ya kifedha.

Zlatan Ibrahimovic anafanya mazungumzo kuregea AC Milan lakini bado makubaliano hayajaafikiwa. Alichezea klabu hio kati ya mwaka 2010 na 2012 na anatafuta klabu mpya baada ya kuondoka LA Galaxy mapema mwezi huu.

Maafisa wa Milan walikutana na ajenti wa Ibrahimovic Mino Raiola jana. Milan wanaaminika kuwa tayari kumpa mchezaji huyo wa miaka 38 mkataba wa miezi 18 lakini matarajio yake ya mshahara yanaonekana kuwa suala kuu.

Mohamed Salah na Andrew Robertson watakosa mechi ya Liverpool na Crystal Palace jumamosi baada ya kukosa kupona majeraha ya miguu. Wachezaji hao wawili wameweza kupumzika wakati wa mapumziko ya kimataifa baada ya kuwachwa nje ya timu zao za taifa lakini ziara ya Selhurst Park inaonekana imekuja mapema.

Jurgen Klopp pia amepata pigo kwa kuwa huenda Joel Matip pia akakosa mechi hiyo. Hajacheza tangu watoke sare na Manchester United mwezi mmoja uliopita na hajapona jeraha la goti. Hata hivyo huenda nahodha Jordan Henderson, aliyekuwa mgonjwa akaweza kucheza.

Kocha mkuu wa timu ya raga ya Kenya Sevens Rugby Paul Feeney asubuhi ya leo atakitaja kikosi cha mwisho kwa msimu wa mwaka 2019/20. Timu hio iliregelea mazoezi mapema wiki hii baada ya kupumzika kwa wiki moja baada ya kufuzu kwa michezo ya Olimpiki mwaka 2020. Collins Injera aliyekua na jeraha la bega pia aliregelea mazoezi na kikosi hicho, kinachojitayarisha kwa Dubai na Cape Town Sevens mwezi ujao.