Habari kuu awamu hii, fahamu yanayojiri mida hii- Radio Jambo

Wakulima wa mahindi kaunti ya Trans Nzoia wamelalamikia hatua ya serikali kuendelea kuagiza mahindi kutoka mataifa ya kigeni ilhali wangali na mahindi katika magala yao.

Wanasema hatua ya serikali kununua mahindi kutoka nje ni njiia mojawapo ya kuwahujumu kama wakenya.

Wiki kadhaa zilizopita waziri wa Kilimo Peter Munya alisema serikali itaanza kununua mahindi kutoka mataifa yaliyoko kwenye Jumuiya ya Afrika mashariki ili kukimu wakenya wanaoangamia kutokana na njaa.

Wafanyabiashara wa kubadilisha pesa katika mpaka wa Kenya na Tanzania wa Holili katika kaunti ya Taita Taveta wamelalama kuwa biashara zao zimerudi chini kutokana na hatua ya serikali kuifunga mipaka hiyo.

Kama njia ya kupunguza maambukizi zaidi nchini, serikali ilifunga mipaka ya Kenya na Tanzania kutokana na hatua ya watu kutoka kwa taifa hilo kupatikana na virusi vya corona.

Sherehe za kuadhimisha siku ya EID mwaka huu zitakuwa tofauti na zingine kwani, waislamu kote nchini wametakiwa kuheshimu masharti yaliyowekwa na serikali ili kupunguza maambukizi ya virusi vya corona.

Tayari wakuu wa miungano ya waislamu nchini wanaitaka serikali kufungua baadhi ya misikiti ili kuwaruhusu kuendelea na shughuli zao.

Wafanyakazi katika sekta ya hoteli nchini wanaendelea kulalamikia hatua ya serikali kuchelewesha matokea yao hata baada ya kupimwa. Wafanyakazi hao sasa wanashtumu kituo kikuu kilichokadhibiwa jukumu la kufanyia vipimo watu wakisema wanaendelea kuumia kiuchumi licha ya kuwa baadhi ya wenzao wamerejea kazini.

Watu watano kaunti ya Mombasa wamejeruhiwa vibaya baada ya kushambuliwa kwa upanga maeneo ya Mshomoroni. Wakaazi wa mitaa hiyo wamelalama kutokana ongezeko la utovu wa usalama ambao umekuwa ukishuhudiwa maeneo hayo.