Wazazi wape watoto fursa ya kukuza vipaji! - Sauti Sol

Wasanii wa kikundi cha Sauti Sol wamewapigia watoto walio na vipaji vya usanii debe ili waweze kupata msaada na msukumo wanaohitaji kutoka kwa wazazi wao.

Wasanii hao walizungumza katika kituo cha Radio Jambo siku ya Ijumaa huku wakiwasihi wazazi kukumbuka kuwa tuko katika karne ya ishirini na moja, ambapo watoto wanajinufaisha maishani kupitia vipaji vyao.

"Wazazi hii ni 21st century, sahii mtoto akifanya kitu mzuri msupport na umpe msukumo ili ajikuze." Alisema msanii Bien.

Sauti Sol walikuwa katika ziara yao ya vyombo vya habari huku wakimpigia debe msanii chipukizi, Ben Soul ambaye amejiunga na kikundi cha 'Sol Generation.'

Ben Soul alizindua kibao chake kipya 'Lucy' siku kadhaa zilizopita ambacho tayari kimepokelewa vyema na wakenya na mashabiki Afrika nzima.

Akifurahishwa na jinsi wakenya wamempokea, Ben Soul aliahidi kuzindua nyimbo zaidi kwa mpigo na zitakazo pendeza.

Kila mtu ambaye ameskiza Lucy na anaipenda nashukuru sana na kama una kipaji pale nyumbani tafadhali jitume jitume. Muziki waja kwa wingi. Alisema.

Lakini je msanii haswa kutoka mashinani akitaka kujiunga na Sol Generation atafanya vipi?

"Ukiangalia Ben Soul si wa Nairobi ni wa Embu. Mtu akitutag kwa video yake katika mtandao wa Instagram lazima tuheshimu talent. Fanya video weka instagram and tag any of us tutakuskiza then we'll get back to you." Walisema Sauti Sol.

Katika juhudi za kukuza vipaji mashinani, Sauti Sol walitangaza kuwa wameshirikiana na gavana wa Kakamega kaunti, mheshimiwa Wycliffe Ambetsa Oparanya.

Ushirikiano wao utawawezesha kujenga kituo kikuu cha vijana cha kukuza usanii.