Mwanaume apatikana ameuawa na mwili wake kutupwa Naivasha

Idadi ya watu wanaopatikana wakiwa wameuawa na mili yao kutupwa huko Naivasha imeongezeka hadi nne hii leo, baada ya mwanamme mmoja kupatikana ameuawa na mwili wake kutupwa katika barabara ya Moi North Lake.

Visa viwili vya kwanza viliripotiwa siku ya Jumatatu na siku moja baadaye kisa cha tatu kika ripotiwa ambapo mwili ulipatakina kichakani huku uso ukiwa na majeraha.

Mwili wa mwanamme huyo ulipatikana mikono ikiwa imefungwa nyuma na kulingana wakaazi huenda alinyongwa na waya kabla ya mwili wake kutupwa katika bara bara hiyo.

Kulingana na kiongozi wa eneo hilo Boniface Waiganjo, mwanamme huyo hakuwa stabadhi yoyote ya kumtambua. Aliongeza kuwa watu wote wanne si wakaazi wa eneo hilo na huenda waliuawa mahala kwingine kisha kutupwa eneo hilo.

Wakaazi sasa wanantaka uchunguzi wa kina kufanywa kuhusu mauaji hayo na wahalifu wanaotekeleza unyama huo kukamatwa.

"Hii ni mara ya kwanza tumeshuhudia visa kama hivi eneo hili na tunaomba polisi kuanzisha uchunguzi mara moja," Waiganjo alisema.

OCPD wa Naivasha Samuel Waweru alithibitisha kisa hicho na kusema kuwa mwili umepelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti.

Huku hayo yakiarifiwa shughuli ya kumtafuta mwanamke mmoja huko Mia Mhiu iliishia majonzi baada ya mwili wake ulokuwa ukioza kupatikana umefungiwa nyumbani kwake.

Inakisiwa kuwa mwanamke huyo aliaga dunia siku ya Jumatatu kabla ya mwili wake kupatikana leo.

Chifu wa eneo hilo alidhibitisha kisa hicho.