Kitany amvua nguo seneta Linturi, hakamani

KITANY
KITANY
Mwanzoni yalikuwa mapenzi ya juu juu. Lakini muda ulivyosonga likachipuka penzi nzito likanoga na kuyeyusha damu na kujikita nyoyoni.

Mwanamke, wanasema hupenda na moyo wake wote. Marrianne Kitany hajasazwa katika kitengo hiki.

Alipata wa mliwaza na kumtomasa roho na kumfanya nywele kusimama tisti utosini. Na angedekeza kipenzi chake kipya Seneta Mithika Linturi kwa kumtunuku chochote kilicho sisimua mtima wake. Pesa hazikuwa hoja.

Huku akitabasamu, mara tena kuvalia sura ya kazi, Kitany aliambia mahakama siku ya Jumatano vile hamu yake kujenga boma ilifanya atumiye mamilioni ya pesa, hatua ambayo anajutia kwa sasa.

Hiyo picha au mandhari ambayo Kitany, aliyekuwa msimamizi wa afisi ya Naibu Rais William Ruto, alieleza katika mahakama ya talaka akisema vile alimpeleka mpenziwe kwa safari za kujivinjari na hata kumjengea nyumba.

Aliambia mahakama kwamba alitumia takriban shilingi milioni 70 kudhihirisha penzi lake.

Kitany alichora picha ya mwanamke ambaye amepagawa na penzi na aliyejitolea kufanikisha mshikamano katika familia yake, iliyojumuisha wanawe watatu kutokana na mahusiano yake ya awali. Ana watoto watatu kutokana na ndoa yake ya kwanza.

Alipeleka familia yake ya watu wanane kwa likizo ya kimataifa iliogharimu malioni ya pesa, alijengea wazazi wa Seneta Linturi nyumba na kuchangia katika ujenzi wa maboma yao mawili ya kifahari.

Kitany aliyeonekana mtulivu mahakamani hakusanza jambo lolote, alimwaya mtama bila kujali uwepo wa kuku. Alisema kwamba walipokutana mara ya kwanza mwaka 2014, angetoa kiasi kikubwa cha pesa kufadhili hafla kadha wa kadha.

Alidai kwamba wakati mmoja mwaka 2014 alimpa Linturi shilingi laki mbili kulipia kodi ya nyumba hatua iliopelekea Linturi kuhamia nyumbani kwake (Kitany) mtaani Kileleshwa Nairobi.

Walipeleka wanao wote Zanzibar mwezi Agosti ili wazoeane kwa sababu walikuwa waanze kuishi pamoja.

Kitany alisema waliwatuma dadake na bwanake pamoja na wanao ili wapate muda wa kushikamana na mpango wao ukafua dafu.

Pia aliambia mahakama kwamba alimshawishi Linturi kumtafutia bintiye shule nchini Australia ambako mwanawe Kitany wa kiume alikuwa akisomea ili watoto wao wasione kana kwamba kuna ubaguzi wa aina yoyote, kwamba baadhi yao wanasomea Kenya na wenzao wanasomea ng’ambo.

Disemba .mwaka huo familia yote ya watu saba walienda ;nchini Australia kwa likizo ya Krismasi ambako watoto wengine na Linturi walikutana na mwanawe Keitany na kutangamana naye.

“Mheshimiwa nilitumia jumla ya shilingi milioni 11 kwa likizo yote iliodumu zaidi majuma mawili na kuzuru miji kadhaa ikiwemo Perth na Sydney,” Kitany alisema.