Matiang'i aonya wanasiasa wanaochochea umma dhidi ya Sensa

Matiang.i
Matiang.i
Waziri wa usalama Fred Matiang’i ametoa onyo kali kwa wanasiasa dhidi ya kuchochea wananchi kususia zoezi la kuhesabu watu kuanzia siku ya Jumamosi.

Matiang’i alisema zoezi hilo halitahusisha mambo mengi na kwa hivyo halifai kuingizwa siasa.

Waziri alisema Kenya ni nchi ya kisasa na zoezi la kuhesabu watu la mwaka 2019 linafaa kufanyika kwa utaratibu mwafaka.

“Na wahimiza viongozi, hasa wanasiasa, kuunga mkono zoezi la kuhesabu watu. Hili ni zoezi la moja kwa moja na tuachie swala hilo hapo. Wacha tuliendeshe kwa adabu,” Matiang’i alisema.

Matiang’i alizungumza siku ya Alhamisi baada ya mkutano wa mwisho wa jopo la mawaziri linaloendesha zoezi la kuhesabu watu la mwaka huu. Alisema serikali inafahamu na inaendelea kupiga msasa shughuli za wanasiasa ikiwemo mikutano ambayo huenda ikatumiwa kuchochea wananchi.

“Tuna tathmini shughuli zao. Tunajua mikutano iliofanyika jana usiku. Mwishowe utakabiliwa kisheria.Tujiepushe na njama kama hizi,” Alisema.

Waziri alikuwa ameandamana na mawaziri wengine Ukur Yatani (Fedha), Joe Mucheru (ICT) na mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya takwimu nchini (KNBS) Zachary Chege. Serikali ilithibitisha kuwa mipango ya zoezi la kuhesabu watu imekamilika.