Rais Kenyatta aomboleza kifo cha mtetezi wa haki za wanawake Kamla Sikand

Rais Uhuru Kenyatta ametuma risala za rambi rambi kwa jamaa, ndugu na marafiki wa mmoja wa mtetezi na mwanaharakti wa haki za wanawake hapa nchini marehemu Kamla Sikand ambaye alifariki Jumatatu.

Katika risala yake, Rais alisema marehemu Sikand alikuwa kiongozi jasiri, mwerevu na shupavu. Alisema marehemu Sikand alikuwa shujaa wa kutetea haki za wanawake na aliyeamini kwa dhati kuhusu hadhi na uadilifu wa binadamu.

 “Ni kwa sababu hii ambapo kama nchi tulimtunuku heshima kama mmoja wa chimbuko la wanawake viongozi,” kaongeza kusema Rais.

Rais Kenyatta alisema marehemu Sikand alijishughulisha mno na juhudi za kutunga katiba ya mwaka wa 2010 hapa nchini akiwa mjumbe katika kongamano la Bomas.

Rais Kenyatta alisema akiwa mtetezi wa haki za binadamu na mshirika wa kampeini dhidi ya ufisadi, marehemu Sikand alitekeleza jukumu kubwa kama mwanachama wa kamati ya kitaifa ya kuongoza harakati za kukabiliana na ufisadi ambapo alizuru sehemu nyingi nchini akielimisha  wananchi kuhusu uovu wa ufisadi.

“Kama taifa tumepoteza kiongozi shupavu, mtetezi wa haki za wanawake na kiongozi aliyepigania jamii isiyokuwa na ufisadi. Alikuwa mmoja wa viongozi wachache wa wanawake waliobobea na walioweka msingi wa harakati za kuwapa shime wanawake na kuleta usawa katika jamii,” kasema Rais.

 Kama mwanachama wa Baraza la Kitaifa la Wanawake Nchini, kundi la Wanawake Wafanyibiashara na Muungano Kisiasa wa Wanawake, Rais alisema Kamla alijitambulisha kuwa mzalendo halisi ambaye alikuwa kielelezo kwa wanawake wengi wachanga.

Rais alimuomba Mwenyezi Mungu kuipa familia, jamaa na marafiki wa marehemu Kamla Sikand nguvu ya kustahimili msiba huo.

-PSCU