Uhuru aonya maafisa wa forodhani

UHURU
UHURU
Maafisa wa Halmashauri ya Bandarini nchini KPA wana sababu ya kuwa na hofu baada ya rais Uhuru Kenyatta kutoa onyo kali kuhusu mienendo ya baadhi yao.

"Raslimali ya umma ni mali ya wakenya sio ya viongozi kujitajirisha,  jukumu la viongozi ni kulinda raslimali hizo kwa niaba ya wakenya. Hilo pekee," Uhuru alisema.

Alizungumza katika bandari ya Mombasa alipozindua safari ya kwanza ya kuuzwa kwa mafuta kutoka Kenya. Uhuru alisema kwamba hatalegeza kamba katika vita dhidi ya ufisadi. Aliwakemea maafisa wakuu wa KPA kwa utepetevu katika kukabiliana na ulaji rushwa katika bandari. Kiongozi wa taifa alisema kwamba taifa la Kenya ni tajiri lakini watu wachache wanataka kujizolea mali wao binafsi.

Uhuru alisema kwamba amepokea taarifa za ujasusi kuwa baadhi ya maafisa wa KPA wanapanga njama ya kuwepo kwa mgomo baridi katika bandari hiyo hatua ambayo huenda ikazorotesha usalama na afya ya wananchi.

“Hata hapa bandarini, rafiki zangu, tunachunguza na tunatazama.”

Alisema palikuwepo njama ya kuchochea mgomo baridi bandarini ili kulemaza shughuli katika eneo hilo. “Ni wakati wa migomo kama hii ambapo shughuli za kihalifu hutekelezwa huku bidhaa haramu zikiingizwa nchini na zingine kusafirishwa nje ya nchi,” alisema.

Uhuru alikwa akizungumza wakati wa hafla ya kuafikiwa ndoto ya Kenya kuwa miongoni mwa mataifa yanayouza mafuta ulimwenguni siku ya Jumatatu. Kenya siku ya Jumatatu ilisafirisha shehena ya mapipa 200,000 ya mafuta yasiyosafishwa kutoka kaunti ya Turkana iliyonunuliwa na kampuni ya ChemChina iliyoko Uingereza, yenye thamani ya shilingi bilioni 1.2, bei ambayo iko juu kuliko ile ambayo ilikuwa imetarajiwa.

Kenya inatumia shehena hii ya kwanza ya mafuta ya petroli ambayo bado hayajasafishwa kama kigezo cha kupima soko la ulimwengu la bidhaa hiyo kabla kuongeza utoaji wa mafuta yake kwa kiwango kikubwa cha kibiashara. Celsius Riga, ambalo ndilo jina la meli iliyobeba shehena hiyo ya mafuta ya petroli ambayo bado hayajasafishwa kutoka Kenya kuelekea Malaysia, iling’oa nanga kutoka Bandari ya Mombasa muda mfupi kabla ya saa sita mchana leo, safari ambayo ilianzishwa rasmi na Rais Uhuru Kenyatta.

Rais Kenyatta alisema usafirishaji wa shehena hiyo ya mafuta ya petroli ni hatua kubwa kwa nchi ya Kenya ambayo sasa imejiunga na mataifa yanayouza mafuta ulimwenguni. “Ninajivunia kusema kwamba safari ya Kenya ya utoaji na uuzaji wa mafuta ya petroli na gesi imeanza rasmi. Kuanzishwa rasmi kwa usafirishaji wa shehena ya kwanza kunaashiria ukurasa mpya kwa taifa la Kenya, na mwanzo mpya wa utajiri kwa Wakenya wote,” kasema Rais Kenyatta.

Rais alisema kwamba Serikali imejitolea kuhakikisha maendeleo bora yanaafikiwa kupitia matumizi ya busara ya raslimali nchini.

“Tutahakikisha ya kwamba maliasli ya Kenya inatumiwa kwa njia ambayo itakuwa ya manufaa ya hali ya juu bila kuhatarisha maslahi ya vizazi vijavyo,” kasema Rais.

Mpango wa Kenya wa Majaribio ya utoaji Mafuta ulianza mwezi Juni mwaka jana, hii ikiashiria mwanzo wa safari ya Kenya kuelekea kuwa taifa ambalo limekuza kikamilifu raslimali zake za mafuta na gesi.  Rais Kenyatta alielezea kwamba Mpango wa Kenya wa Majaribio ya utoaji Mafuta umedhihirishia soko la ulimwengu kuwa Kenya ina ujuzi na muundomsingi unaohitajika kuwezesha utoaji mafuta kwa viwango vya kibiashara.

Rais alisema awamu itakayofuata mafanikio ya mradi huo wa majaribio ya utoaji wa mafuta itakuwa uimarishaji wa nyanjani ambao utahusisha usafirishaji wa mafuta kwa njia ya bomba kutoka Lokichar hadi katika bandari mpya ya Lamu.