Ukatili wa baba! Msichana wa miaka 15 aficha mimba ya babake kwa miezi 5

MIMBA
MIMBA
Mahakama mjini Nanyuki siku ya Jumatano iliambiwa vile msichana wa miaka 15 alificha uja uzito kwa miezi mitano kwa hofu ya kuauwa na babake wa kambo anayedaiwa kumnajisi.

Babake wa kambo anadaiwa kumtishia kwamba atamuua ikiwa angefichua uja uzito aliokuwa amebeba ulikuwa na babake. Mwanamume huyo ameshtakiwa kuwa kati ya mwezi Aprili na Septemba mwaka jana, alimnajisi msichana mwenye umri wa miaka 15 nyumbani kwake katika kijiji cha Magutu, Laikipia Mashariki. Alikanusha mashtaka, akidai kusingiziwa na mkewe na kakake mkwe ili wachukuwe umiliki wa shamba lake.

Mamake msichana huyo aliambia mahakama aligundua kwamba tumbo la bintiye lilikuwa limekuwa kubwa. Alipomshawishi azungumze msichana alifichua kwamba alikuwa amenajisiwa na babake wa kambo miezi iliopita wakati mamake alikuwa ameenda hospitalini.

“Binti yangu alinieleza kwamba wakati nilikuwa sipo babake aliwatuma wenzake wadogo kwenda kuchota maji mtoni na walipoondoka, alimvuta ndani ya nyumba na kumnajisi, kisha alimuonya dhidi ya kuambia mtu yeyote na kwamba angemuua,” Mama huyo wa watoto wanane aliambia mahakama huku akitiririkwa na machozi.

Wakati wa mahojiano, mshukiwa aliambia hakimu mkaazi Vincent Mativo kwamba hakuwa na sababu ya kumnajisi bintiye wa kambo, na ilhali alimshughulikia msichana huyo kama mwanawe.

“Nimekuwa nikiwaelimisiha watoto wote wanane bila ubaguzi, licha ya kwamba watatu pekee ndio wanangu. Hakuna vile ningefikiria kufanya kitendo kama hicho na mwanangu, huu wote ni uongo," Alisema.

Mahakama iliambiwa kwamba msichana huyo alijifungua mtoto huyo kabla ya siku zake kutimia na mtoto akafariki katika Hospitali ya Rufaa ya Nanyuki. Mhasiriwa Kwa sasa anaendelea kupokea ushauri nasaha kuhusiana na tikio hilo.

Kesi inaendelea.