Rais Mtaafu Moi alazwa katika Nairobi Hospital

MOI
MOI
Rais mstaafu Daniel arap Moi amelazwa katika Nairobi Hospital kwa kile familia imesema ni uchunguzi wa kimatibabu wa kawaida.

Taarifa zinasema kwamba Moi alilazwa Ijumaa na anatarajiwa kukaa kwa siku kadhaa hospitalini kwa uchunguzi wa kina wa kimatibabu.

"Hakuna jambo la kuhofia. Yuko huko kwa uchunguzi wa kimatibabu wa kawaida anahudumiwa na na daktari wake Dr David Silverstein. Anatarajiwa kusalia huko kwa siku kadhaa ili kuwapa madaktari muda wa kutosha, " Radio Jambo iliarifiwa.

Katibu mkuu wa Kanu Nick Salat amethibitisha kwamba Moi amelazwa hospitalini.

"Ndio, yeye anafanyiwa uchunguzi wa kimatibabu wa kawaida," Salat, ambaye aliteuliwa mnamo Aprili kuwa mwenyekiti wa Shirika la Posta, aliiambia Radio Jambo kwa simu.

Hata hivyo tulipowasiliana na katibu wa mawasiliano wa Moi, Lee Njiru, alikana madai hayo na kusema kwamba hakufahamu kuwa Moi amelazwa hospitalini.

"Niko Nakuru na sina ufahamu kuhusu hizo ripoti. Nitawajulisha nikipata ripoti maalum," Njiru alisema alipopgiwa simu.

Kulazwa kwa Moi kunajiri siku chache tu baada ya Wakenya kusherehekea sikukuu ya Moi Day.