Familia ya Raila na Mjane wa Fidel wazozania mali ya Marahemu Fidel

Taarifa ya familia ya kinara wa upinzani Raila Odinga kwa polisi kuhusu kifo cha ghafla cha mwanao Fidel Odinga imeibua mkwaruzano mkali na mjane wa Fidel na kupelekea swala hili kufika hadi mahakamani.

Katika kesi hii, Mkewe Raila Ida na bintiye Winnie wanataka kumzuia mjane wa Fidel Lwam Bekelle dhidi ya kuwa msimamizi wa pekee wa mali ya marehemu bwanake.

Katika stakabadhi za mahakama zilizofikia gazeti la The Star, Bekelle anasema taarifa alioandika Ida kwa idara ya DCI kuhusiana na kifo cha Fidel ndio msingi wa tofauti zao.

“Naamini kwamba taarifa iliowasilishwa kwa DCI kufuatia kifo cha Fidel Castro Odhiambo Odinga ndicho chanzo cha tofauti zetu ,” Bekelle alisema.

Bekelle anamshtumu mamake mkwe “kwa kuendelea kutoa madai ya uongo, kuchafua majina ya marafiki wa familia na dhidi yake mwenyewe.”

Katika hati ya kiapo, Ida na Winnie wanamshtumu Bekelle kwa kutoroka boma lake mtaani Karen punde tu Fidel alipozikwa na kukatiza mawasiliano na familia ya Odinga.

Pia wanasema kwamba Bekelle alijitenga na juhudi za familia ya Odinga kutaka kupata kilichopelekea kifo cha Fidel.

“Licha ya kwamba kifo cha ghafla cha marehemu kiliacha maswali chungu nzima na juhudi kuanzishwa kubaini nini kilifanyika, Bekelle alijitenga na familia,” Ida na Winne walisema katika hati yao ya kiapo.

Waliendelea kusema: “Bado haieleweki kwanini Bekelle alikuwa na haraka kuondoka na kukatiza mawasiliano na familia, na ilhali pamekuwepo juhudi kadhaa kuwasiliana naye.”

Lakini Bekelle alitaja taarifa hiyo kama “isiokuwa na msingi, ya kukera na yenye hila ”. Alisema Ida ana ripoti ya upasuaji wa mwili wa Fidel.

Fidel ambaye alikuwa mrithi wa kwanza wa mali ya Raila alifariki Januari 4, 2015, baada ya kukesha na rafiki zake wakijistarehesha. Aliacha mtoto mmoja mvulana, Allay Raila Odinga.

Ripoti ya upasuaji wa mwili wa Fidel imesalia siri kufikia leo. Katika stakabadhi za mahakama Ida na Winnie wanatoa sababu kadhaa kwanini mjane huyo hafai kuachiwa usimamizi wa mali ya Fidel.

Kwa mara ya kwanza, wawili hao walisema Fidel alikuwa na watoto mapacha na mwanamke mwingine, msichana na mvulana na ambao pia wana haki kisheria kugawiwa mali yake.

Mama ya mapacha hao ametajwa katika stakabadhi za mahakama kama Phoebe Akinyi Ogweno.

“Mjane wa Fidel amekataa kuwaongeza au kuonyesha nia vile wale watoto wengine watashughulikiwa hali ambayo ilichochea kuchukuliwa kwa hatua hii,” Ida alisema.

Hata hivyo kupitia wakili wake Bekelle aliataja matamshi ya mamake mkwe kama ubunifu wake tu na kwamba mapacha hao walizaliwa miezi sita baada ya Fidel kuaga.

“Katika vyeti vya kuzaliwa vya watoto hao vilivyojumuishwa kwenye stabadhi za kesi jina la baba wao halijatajwa. Kwa hivyo stakabadhi hizo hazionyeshi uhalisi wa baba yao,” Bekelle alisema.

Alipuuzilia mbali madai ya Ida kuwa Fidel aligharamia mahitaji ya watoto hao kwa sababu hawakuwa wamezaliwa wakati Fidel akifariki. Mjane huyo pia anadai kuwa familia ya Odinga haimsaidi mwanawe na kukanusha madai kuwa ameacha shule.

Mvutano huu umefichua mali ya thamani ya mabilioni ya pesa ilioachwa na mwanwe wa kwanza wa Raila, aliyefariki akiwa na umri wa miaka 41.