Watu 8 wakamatwa Nyandarua kwa madai ya wizi wa mtihani wa KCPE

Polisi mjini Nyandarua wamewakamata washukiwa nane wanaokisiwa kuhusika katika njama ya wizi wa mtihani unaondelea wa KCPE.

Nane hao walikamatwa katika shule ya Hezta Schools, Ol Kalou Jumatano jioni baada ya uchunguzi uliofanywa na maafisa wa DCI na wa kutoka wizara ya elimu.

Kaunti commissioner wa Nyandarua, Boaz Cherutich, kamanda wa kaunti Gideon Ngumi, na mkurugenzi wa elimu Nelson Sifuna pamoja na maafisa wengine wa elimu na wa kitengo cha polisi walikuwemo katika zoezi hilo.

Waliokamatwa ni pamoja na meneja Robert Simba Odara, msimamizi wa mitihani kutoka KNEC, William Mbugua, wasimamizi wawili wa mitihani ndani ya kituo hicho, Dorcas Wahome na Dickson Gachau. Wanne hao watafikishwa mahakamani.

Wengine waliokamtwa na wanasaidia na uchunguzi ni Tabitha Wambui anayesimamia shule hiyo ya Hezta, meneja wa shule, Musa Mirobi pamoja na walimu wa shule hiyo.

Makaratasi kadhaa ya tishu na vifutio vilivyotumika katika wizi wa mtihani pia vilipatikana huku simu kadhaa zilizotumika kutekeleza kitendo hicho pia zikibebwa ili kusaidia na upelelezi.

Cherutich alisema maafisa wa usalama waliotumwa kuchunga kituo hicho walishuku kuwa kuna jambo liliso sawa na kupiga ripoti. Alisema wizi huo ulikuwa umepangwa vyema na usahihi wa kijeshi.

Aliongeza kuwa wahusika watapambana na mkono mrefu wa sheria ili iwe funzo kwa wengine.