Raia wawili wa kigeni wapewa muda wa siku tatu kulipa bili ya hoteli

Botswana
Botswana
Raia wa kigeni wamepewa hadi masaa 72 kulipa deni la shilingi 382,832 au kukabiliwa kisheria.

Wawili hao ambao  ni mwanaume na wakili wake kutoka Botswana wamekuwa wakiishi katika hoteli ya Emerald eneo la Westlands.

Wakiwa kizimbani, hakimu Joyce Gandani aliwaamuru Sejero Marapel na Laetsang Kopolerero kulipa deni hilo kabla ya kuondoka hotelini.

Kulingana na mashtaka hayo, wawili hao wanadaiwa kiasi cha shilingi 382,832 kati ya Septemba 20 na Oktoba 31.

Kopolerero alisafiri nchini pamoja na wakili wake pamoja na rafikiye anayejulikana kama Mpumellelo kwa ziara ya kibiashara.

Hata hivyo Marapel aliiambia korti kwamba Kopolerero alitakikana kulipa bili zote zao.

Marapel alijitetea kwamba alikuwa ameagizwa kushuhudia Kopolerero akitia sahihi mikataba.

Lakini baada Kopolerero akabaini kwamba alikuwa amelaghaiwa mamilioni ya fedha na mtu aliyedai kuwasaidia.

Hapo ndipo alipoamua kuwa kila mmoja alipe bili zake, kinyume na alivyoahidi awali.

Mpumellelo anasemekana kutoroka baada ya kuwahadaa kwamba angeenda kusaka pesa za kulipa bili za hoteli.

Marapel aliirai korti impe nafasi ya kuwasiliana na dadake anayeishi California ili awasaidie na fedha za kulipa hotelini.

"Tukizuiliwa itakuwa vigumu sana kwetu kupata msaada, naomba korti iamuru nipate kuwasiliana na watu wangu," alisema.

Kesi hiyo itasikilizwa tena Ijumaa.