Afisa mkuu wa uchaguzi katika eneo bunge la Kibra Beatrice Muli alitangaza matokeo rasmi ya uchaguzi huo siku ya Ijumaa asubuhi.
Akihutubia wananchi punde tu baada ya uchaguzi kutangazwa Imran aliahidi kushirikiana na wapinzani wake wote ili kuleta maendeleo katika eneo bunge la Kibra.
Imran alisema yeye ni mbunge wa kwanza wa ‘Handshake’na kuapa kuunganisha jamii zote katika eneo la Kibra bila kujali vyama vyao vya kisiasa.
“Mimi ni mtoto wa kwanza wa Handshake kati ya baba Raila Odinga na Rais Uhuru Kenyatta, ajenda yangu kuu itakuwa kuunganisha jamii zote katika eneo bunge la Kibra na kutumikia wananchi wote,” Imran alisema.
Alipongeza wanachama wa vyama vingine chini ya Handshake kwa kumuunga mkono.
Imran aliungwa mkono na wanachama wa Jubilee Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru, Maina Kamanda mbunge maalum, Spika wa Kaunti ya Nairobi Beatrice Elachi na aliyekuwa mbunge wa Dagoreti South Dennis Waweru.